Je,vikosi ziada Afghanistan vitasaidia kuleta utulivu?
30 Januari 2009Wachambuzi hao wanauliza iwapo kupelekwa kwa wanajeshi ziada Afghanistan kutasaidia kuleta utulivu katika nchi hiyo au kutachochea tu chuki zaidi miongoni mwa Waafghanistan dhidi ya vikosi vya kigeni?
Rais mpya wa Marekani Barack Obama,atapaswa kujiamulia kwa umbali gani atie maanani hofu za wachambuzi hao,huku serikali yake ikirithi mizozo ya enzi ya George W.Bush.Kwa maoni ya kanali mstaafu wa jeshi la Marekani Andrew Bacevich, itakuwa busara kwa Barack Obama kuzingatia vizuri kabla ya kuchukua hatua na kuifanya Afghanistan "Vita vya Obama". Bacevich anasema,ni kweli kuwa Marekani haitaki kuona Afghanistan ikiwa kituo cha wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu wenye azma ya kuwaua Wamarekani. Lakini ana wasiwasi ikiwa ni lazima kuleta mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Afghanistan ili kuhakikisha usalama wa Marekani.
Maoni kama hayo yanazidi kuchomoza katika taarifa rasmi nchini Marekani. Kwa mfano juma lililopita hata Waziri wa Ulinzi Robert Gates alisema, Marekani iwe na malengo ya wastani ya muda mfupi.Hata hivyo Gates aliekuwa na wadhifa huo pia katika serikali ya Bush,ameunga mkono maombi ya Jemadari wa Marekani David McKiernan anaeongoza vikosi vya NATO nchini Afghanistan kupeleka hadi wanajeshi 30,000 ziada katika kipindi cha miezi 12 hadi 18 ijayo.
Obama alipokuwa akipigania uchaguzi wa rais alisema,Afghanistan ipo mstari wa mbele katika vita vya Marekani dhidi ya ugaidi na aliahidi kupeleka brigedi mbili za kiasi ya wanajeshi 7,000 wengine.Wakuu wa kijeshi wa Marekani wanasema,vikosi ziada vitasaidia kulinda usalama wakati wa kufanywa uchaguzi ujao nchini Afghanistan.Na vikosi vya NATO ndio vitaweza kubakia katika maeneo walikotimuliwa waasi na kutakuwepo nafasi ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuanzisha hudumu muhimu ili kuwavutia wakaazi wa maeneo hayo walio chini ya ushawishi wa Wataliban.
Lakini mwanadiplomasia wa zamani wa Uingereza Rory Stewart anasema, nchi za Magharibi zinashughulikia zaidi Afghanistan na hali wanamgambo wa Al-Qaeda katika maeneo ya kikabila nchini Pakistan ni kitisho kikubwa zaidi.Stewart aliesafiri kwa miguu kila pembe ya Afghanistan hapo mwaka 2002 na alieanzisha taasisi ya kusaidia kuufufua mji mkuu Kabul,anaamini kuwa hatimae,ni Waafghanistan wenyewe watakaoweza kuleta utulivu wa kudumu nchini mwao.