Jeshi lazima uasi Madagascar
22 Novemba 2010Waziri Mkuu wa Madagascar, Camille Vital, amesema kuwa jaribio la kuiangusha serikali limezimwa bila ya damu kumwagika, baada ya maafisa 16 wa kijeshi waliohusika na uasi huo wamejisalimisha.
Hapo awali waasi walitangaza kuwa walikuwa wanatwaa mamlaka kutoka kwa kiongozi wa sasa, Andry Rajoelina, ambaye mwaka jana pia alitwaa uongozi kutokana na kuungwa mkono na wanajeshi. Mamia ya Wanajeshi watiifu walionekana wakikusanyika karibu na uwanja wa ndege ambapo waasi walikuwa wameweka kambi yao. Maafisa waasi walikuwa wametangaza kuvunjwa idara zote za uongozi za Madagascar na kusema kuwa wameunda baraza la uongozi la kijeshi.
Waziri Mkuu Vital amesema licha ya kusikika milio ya silaha, hakuna mtu hata mmoja aliyejeruhiwa, na kwamba sasa hali imerejea kuwa shwari katika nchi hiyo.