1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi latumwa kuwatuliza wanafunzi wanaoandamana Eswatini

12 Oktoba 2021

Wanajeshi na polisi wametumwa kwenye skuli kadhaa nchini Eswatini, ambako wanafunzi wamekuwa wakiandamana kudai mabadiliko ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/41ZCo
Eswatini Proteste
Picha: AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa makundi ya kupigania demokrasia, jeshi limetumwa kuwatisha wanafunzi hao, ambao hadi sasa hawajaonesha nia ya kurudi nyuma.

Msemaji wa Mtandao wa Mshikamano wa Swaziland, Lucky Lukhele, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanafunzi 17 walikamatwa jana, akiwemo mmoja mwenye umri wa miaka saba.

Chama cha Kikomunisti cha Swaziland kimesema waandamanaji kumi wamekamatwa na mwanafunzi mmoja amepigwa risasi ya mguu.

Msemaji wa jeshi, Tengetile Khumalo, amekiri kutumwa kwa wanajeshi, lakini amesema jeshi si adui wa raia, bali wametumwa kwa ajili ya kuweka utulivu.

Wanafunzi katika taifa hilo pekee lililosalia na ufalme kusini mwa Afrika, wamekuwa wakisusia masomo na kufanya maandamano kila mara, wakidai kuachiwa huru kwa wanasheria wawili waliokamatwa kwenye maandamano mengine mwanzoni mwa mwaka huu.