Jeshi lamvua madaraka Bashir
11 Aprili 2019"Kamati ya usalama imeamua, ikiwa ni pamoja na majeshi ya ulinzi na wadau wengine, kutekeleza kile kiongozi wa serikali hakuweza kufanya, na kuchukua jukumu kamili la kubadilisha serikali yote katika muda wa mpito wa miaka miwili ambapo majeshi ya ulinzi kimsingi yatachukua uongozi wa nchi na kuzuwia umwagikaji wa damu pamoja na uwakilishi wa kiasi kutoka kamati ya usalama."
Waziri wa ulinzi wa Sudan alitangaza leo kwamba jeshi limempindua na kumkamata rais Omar al-Bashir na kuchukua madaraka ya nchi kwa miaka miwili ijayo kufuatia karibu miezi minne ya maandamno dhidi ya utawala wake. Awad Mohammed Ibn Ouf alionekana katika televisheni ya taifa akivalia sare za jeshi , kufuatia tangazo la hapo kabla , kuhusu " taarifa muhimu, kutoka katika jeshi leo Alhamis.
Ibn Ouf amesema baada ya miaka miwili , uchaguzi huru na wa haki utafanyika.
Amesema amri ya hali ya hatari imewekwa kote nchini kwa muda wa miezi mitatu na kwamba jeshi pia limesitisha katiba ya nchi hiyo, kufunga mipaka na anga ya nchi hiyo.
"Pia natangaza kuundwa kwa baraza la mpito la jeshi ambalo litatawala kwa miaka miwili, kusitisha katiba ya mpito ya Sudan iliyopitishwa mwaka 2005. Natangaza hali ya hatari kwa miezi mitatu na amri ya kutotembea usiku kwa mwezi mmoja, kuanzia saa 4 usiku hadi saa 10 alfajiri. Nafunga anga ya Sudan kwa masaa 24 pamoja na bandari zote za kuingilia Sudan hadi itakapotangazwa tena. Pia navunja taasisi ya rais na bunge."
Idara za usalama pia zimetangaza kuwaacha huru wafungwa wote wa kisiasa. Pamoja na hayo waandamanaji wamekataa tangazo hilo la jeshi na kusema maandamano yataendelea kwa kuwa hicho ndio walikuwa wakipambana nacho. Maelfu ya watu waliingia katika mitaa ya mji mkuu Khartoum leo kuandamana dhidi ya tangazo hilo la jeshi kwamba rais Omar al-Bashir ameondolewa na nafasi yake itachukuliwa na baraza la mpito litakaloongozwa na jeshi.
Hali ya waandamanaji ambao hapo kabla walikuwa wakishangilia iligeuka kuwa hasira , wengi wakiimba , anguko jingine, wakichukua nyimbo walizokuwa wakiimba hapo kabla za kumpinga Bashir.