1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Jeshi lamtangaza Brice Nguema kama kiongozi wa mpito Gabon

31 Agosti 2023

Viongozi wa kijeshi waliochukua madaraka nchini Gabon wamemtangaza mkuu wa kitengo cha walinzi wa rais, Brice Clotaire Oligui Nguema, kama kiongozi wa mpito nchini humo.

https://p.dw.com/p/4VmEB
General Brice Clothaire Oligui Nguema
Picha: Gabon24/AP/picture alliance/dpa

Brice Nguema, kulingana na ripoti za vyombo vya habari ni binamu wa rais aliyeondolewa madarakani Ali Bongo.

Msemaji wa linalojulikana kama baraza la mpito, kupitia shirika la habari la serikali la Gabon 24, alimtangaza Nguema kama rais wa mpito jana jioni.

Saa chache baada ya viongozi wa kijeshi kutwaa mamlaka, Rais Ali Bongo alionekana kwenye ukanda wa video akitoa wito wa usaidizi.

Soma pia:  Ali Bongo alidhani angezuwia Gabon, anaweza kuwa alikosea

Bongo amewataka raia wa Gabon "kupiga kelele" na kueleza kuwa amezuiliwa kinyume cha sheria katika maakazi yake.

Kundi la maafisa wa ngazi ya juu jeshini wameiambia televisheni ya taifa kuwa Bongo anatuhumiwa kwa uhaini mkubwa.

Wakati hayo yanaarifiwa, mashirika ya kikanda na kimataifa yameonyesha wasiwasi wao juu ya kinachoendelea huko Gabon.

Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Afrika walaani mapinduzi

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki
Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa FakiPicha: Simon Maina/AFP

Ufaransa na Umoja wa Afrika umelaani mapinduzi hayo na kuhimiza suluhu ya amani kwa mzozo uliojitokeza baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki ameyataja mapinduzi hayo ya kijeshi katika taifa hilo koloni la zamani la Ufaransa kama ukiukaji wa wazi wa sheria ikiwa ni pamoja na mkataba wa Afrika kuhusu uchaguzi, demokrasia na utawala.

Faki ametoa wito kwa jeshi la Gabon kuhakikisha usalama wa Ali Bongo, jamaa zake na baadhi ya maafisa waliokuwa wakimuhudumia.

Soma pia:  China yataka usalama wa Bongo uhakikishwe

Mwenyekiti huyo wa kamisheni ya Umoja wa Afrika ameongeza kuwa, watendaji wa kisiasa, kiraia na kijeshi katika taifa hilo wanapaswa kutoa kipaumbele kwa amani na kurudi kwa haraka kwa utawala wa kidemokrasia.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ameelani mapinduzi hayo yaliyofanyika kama njia ya kutatua mgogoro wa baada ya uchaguzi.

Kupitia taarifa, Guterres ametoa wito kwa wahusika wote kushiriki katika mazungumzo jumuishi na kuhakikisha kuwa utawala wa kisheria na haki za binadamu zinaheshimiwa.

Jeshi lafuta matokeo ya uchaguzi na kufunga mipaka ya nchi

Jeshi lilitwaa madaraka nchini Gabon mapema jana Jumatano. Maafisa wa kijeshi walitangaza kwenye televisheni ya kitaifa kuwa taasisi zote za serikali na matokeo ya uchaguzi yamefutwa kutokana na udanganyifu na kwamba mipaka ya nchi hiyo imefungwa.

Muda mfupi kabla, tume ya uchaguzi ilimtangaza Ali Bongo, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2009, kama mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 26.

Raia wa Gabon wakisherehekea mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Ali Bongo
Raia wa Gabon wakisherehekea mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Ali BongoPicha: AFP/Getty Images

Nguema, ambaye sasa ndio kiongozi wa mpito, alikuwa mkuu wa kitengo cha walinzi wa rais tangu mwaka 2020. Kulingana na ripoti ya Jeune Afrique, mamake alikuwa na uhusiano wa damu na babake Ali Bongo, Omar, aliyetawala nchi hiyo kutoka mwaka 1967 hadi kifo chake mwaka 2009.

Na kama ilivyo kwa familia ya Bongo, inayoaminika kuwa moja ya familia tajiri duniani, Nguema amehusishwa na kashfa za ufisadi. Anadaiwa kumilika mali kadhaa nchini Marekani.

Ali Bongo, rais aliyeondolewa madarakani, anatuhumiwa kwa uhaini mkubwa. Mwanawe wa kiume, Nouredine Bongo, pia amekamatwa. Familia ya Bongo imeitawala Gabon kwa zaidi ya miaka 50 licha ya kufanyika kwa uchaguzi mara kwa mara nchini humo.

Nchi hiyo yenye idadi ya watu wapatao milioni 2.3, wengi wanaishi katika umaskini mkubwa licha ya Gabon kuwa na utajiri wa mafuta.