Jeshi lakanusha kutokea mapinduzi Lesotho
31 Agosti 2014Thabane amekaririwa akiliambia shirika la habari la BBC kwamba "Ameondolewa madarakani sio na wananchi bali na vikosi vya jeshi la ulinzi na kwamba jambo hilo sio halali."
Amesema kwamba amekwenda Afrika Kusini wakati wa asubuhi na atarudi nchini mara tu maisha yake yatakapokuwa hayako tena hatarini na kwamba hatorudi Lesotho kuwawa.
Waziri mmoja wa serikali ameliambia shirika la habari la AFP kwamba jeshi la Lesotho limechukuwa udhibiti wa makao makuu ya polisi na makaazi ya waziri mkuu katika mji mkuu wa Maseru mapema Jumamosi alfajiri lakini baadae waliondoka.
Jeshi lilidhibiti makao makuu ya polisi
Waziri huyo wa michezo na kiongozi wa chama cha Taifa cha Basotho Thesele Maseribane amesema jeshi la ulinzi,vikosi maalum vya Lesotho vimedhibiti makao makuu ya polisi.
Amesema aliarifiwa kwamba kamanda wa jeshi alikuwa akimtafuta yeye,waziri mkuu na naibu waziri ili awapeleka kwa mfalme jambo ambalo anasema linaamanisha kuna mapinduzi.
Maseribane amesema watu waliokuwa na bunduki walikuwa wakiranda katika mji mkuu lakini alikuwa hana taarifa kuhusu maafa na amelishutumu jeshi kwa kukwamisha matangazo ya radio na mawasiliano ya simu.
Pia amemshutumu Naibu Waziri Mkuu Mothetjoa Metsing kiongozi wa chama cha Lesotho Congress for Demokrasia (LCD) ambacho ni mshirika katika serikali ya mseto kwa kuhusika katika jaribio hilo la kunyakuwa madaraka.
Amesema kuna taarifa fulani za kijasusi kwamba yeye ni sehemu ya mapinduzi hayo.
Mzozo ulikuwa ukifukuta
Chama cha LCD ni sehemu ya serikali ya mseto inayoyumba ambayo imekuwa ikitawala tokea kumalizika kwa uchaguzi miaka miwili iliopita.
Lakini kutokana na kuzidi kukatishwa tamaa na Thabane chama hicho kiliapa miezi michache iliopita kuunda serikali mpya na kumuondowa madarakani waziri mkuu katika taifa hilo la kifalme lililozungukwa kabisa na Afrika Kusini linalojiita "ufalme wa mbinguni."
Thabane alilivunja bunge kwa baraka za Mfalme Letsie III ambaye ameitawala nchi hiyo ya ufalme unaotambuliwa kikatiba tokea mwaka 1996 na hiyo kumuwezesha kuepuka kura ya kutokuwa na imani naye.
Baada ya mazungumzo ya dharura mwezi wa Juni vyama vinavyounda serikali ya mseto nchini humo kikiwemo cha Thabane cha All Basotho Convention (ABC) vilikubaliana kuendelea kushirikiana.
Waziri wa michezo baadae alisema jeshi liliondoka makao makuu ya polisi na kurudi kambini lakini limeyachukuwa magari yote ya polisi.
Maseribane amesema amekimbia nyumbani kwake baada ya kupata onyo la kuwepo kwa mapinduzi hayo na amekataa kusema mahala alipo.Amesema yeye na waziri mkuu bado wamo katika serikali ya mseto,waziri mkuu bado yuko madarakani na bado kuna hatari kubwa nchini humo.
Jeshi lakunusha mapinduzi
Msemaji wa jeshi la ulinzi Ntlele Ntoi amekanusha kwamba kumetokea mapinduzi nchini humo ambapo amesema kamwe hakukuwa na mapinduzi na katu hakutokuwa na mapinduzi yatakayofanywa na jeshi nchini humo.
Ameliambia shirika la habari la AP kwamba hali katika mji mkuu wa Lesotho sasa imerudi katika hali ya kawaida na kwamba watu wako katika pirikapirika zao kama kawaida.
Ntoi amesema jeshi lilikuwa limepata taarifa za ujasusi kwamba polisi ilikuwa imepanga kuwapatia silaha makundi yatakayoshiriki katika maandamano yaliopangwa kufanyika Jumatatu yalioitishwa na chama kimojawapo cha serikali ya mseto cha (LCD) na jeshi limewapokonya silaha polisi katika mji mkuu wa Maseru ili kuepusha umwagaji damu.
Amesema jeshi halijui iwapo maandamano hayo yataendelea kufanyika hapo Jumatatu.
Mizozo ya kisiasa sio jambo geni nchini Lesotho.
Hapo mwaka 1986 utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini ulichochea mapinduzi nchini humo ili kuizuwiya nchi hiyo isitumiwe kuwa kambi ya chama cha ANC na wanaharakati wengine.
Mwaka 1998 kufuatia vurugu za uchaguzi Afrika Kusini na Bhotswana vilifanya uvamizi uliopelekea kuharibiwa kwa mji mkuu wa nchi hiyo.
Katika miongo ya hivi karibuni kumekuwepo na majaribio kadhaa ya mauaji ya kisiasa.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP
Mhariri : Sudi Mnette