Jeshi lapambana na wafuasi wa upinzani nchini Zimbabwe
1 Agosti 2018Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamesema uchaguzi wa Zimbabwe umefanyika katika "mazingira yasiyo sawa" mnamo ambapo wafuasi wa chama cha upinzani cha vuguvugu kwa ajili ya mageuzi ya kidemokrasia MDC wakiandamana kupinga kuwepo na hila zinazofanywa na tume ya uchaguzi.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wamesema katika ripoti yao kwamba "mazingira ya kisiasa yameimarika" lakini mchakato mzima umekuwa uwanja usio sawa na kukosa imani. Mkuu wa waangalizi wa umoja huo Elmar Brok amesema "kulikuwa na jitihada za kudhoofisha uhuru wa ridhaa ya kujieleza wa wapiga kura kupitia ushawishi, vitisho vyepesi, shinikizo na ushurutishaji, ili kuhakikisha wanakipigia kura chama tawala.
"Kwa nyakati nyingi, maandalizi, ufadhili, vyombo vya habari na pengine sio katika kuhesabu kura, kulikinufaisha chama tawala", Brok aliliambia shirika la habari la AFP. Mnangagwa mwenye miaka 75 ameahidi uchaguzi huru na haki baada ya kumuondoa kijeshi Robert Mugabe madarakani.
Hata hivyo waangalizi hao wamesema kwa ujumla uchaguzi umeendeshwa kwa amani ukilinganisha na kipindi cha nyuma lakini wanashangaa kwa nini kura za urais zilihesabiwa kwanza na zinatangazwa mwisho. Waangalizi wa Umoja wa Ulaya na wale wa Marekani kwa pamoja wametoa mwito wa kutangazwa haraka kwa matokeo hayo, ambapo mkuu anayeongoza ujumbe wa Marekani rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ameonya kwamba matokeo yakichelewa zaidi kunaibuka maswali juu ya mchakato mzima wa uchaguzi.
Nayo jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, katika ripoti yake ya awali imesema kampeni na uchaguzi vimeendeshwa katika njia ya amani na taratibu na kwa sehemu kubwa sheria za Zimbabwe ilizingatiwa. Imetoa wito wa mgombea yoyote aliye na malalamiko "kujizuia na hatua zozote za vurugu". Katibu mkuu wa MDC Douglas Mwonzora ametoa kauli ifuatayo.
"Kitu ambacho si huru na haki hakiwezi kukubalika. Lakini tulichosema kama MDC ni kwamba tutapambana kwa kutumia sheria, na kuna mambo mawili, matatu ambayo tunaweza kuyafanya kisheria. La kwanza ni kwenda mahakamani kama tunadhani tumekusanya ushahidi wa kutosha. La pili ni kwamba kisheria tunaruhusiwa kuandamana na kutoa pingamizi. Njia nyingine ni shinikizo la kidiplomasia na kadhalika," amesema Mwonzora.
Ikiwa hakuna mgombea urais atakayeshinda angalau kwa asilimia 50 katika duru ya kwanza, duru ya pili imepangwa kufanyika Septemba 8. Tume ya uchaguzi imeonya kwamba matokeo ya mwisho ya mshindi wa urais huenda yasijulikane hadi siku ya Ijumaa au Jumamosi, lakini matokeo ya awali yanaweza kutangazwa baadaye hivi leo.
Wakati huo huo mamia ya wafuasi wa upinzani waliojawa na hasira wamekusanyika nje ya tume ya uchaguzi ya Zimbabwe na kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia ambao wamefyatua gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya wakati matokeo rasmi ya mshindi wa urais yakisubiriwa. John Moyo ni mfuasi wa MDC "Tumechoka! Zimbabwe ni ya kila Mzimbabwe. Sote ni Wazimbabwe, tumeumia sote, tulipigana vita sote, wazazi wetu walikufa, kila mmoja alikufa kwa ajili ya nchi hii. Kwa hiyo tunahitaji mabadiliko. Imetosha!, nchi hii si ya watu wawili tu, ni ya kila raia wa Zimbabwe".
Wafuasi hao katika mji mkuu wa Harare walirusha mawe na kuikataa serikali, wakishusha bango lenye picha ya rais Mnangagwa lenye kauli mbiu ya kampeni "sauti ya watu ni sauti ya Mungu". Mtu mmoja ameripotiwa kupoteza maisha baada ya kupigwa risasi na vikosi vya usalama.
Chama tawala nchini humo cha ZANU-PF kimeshinda viti vingi katika bunge la nchi hiyo, kwa mujibu wa matokeo yaliyokwisha kutolewa na tume ya uchaguzi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo