1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi laivamia radio Madagascar : Je! SADC itafanikiwa?

Admin.WagnerD24 Julai 2012

Radio ya Upinzani nchini Madagascar, Free FM imesitisha kurusha matangazo yake kutokana na vitisho kutoka Jeshi la serikali nchini humo, vilivyotolewa baada ya kutokea uasi mwishoni mwa juma.

https://p.dw.com/p/15e5I
Kiongozi wa sasa wa Madagascar, Andry Nirina Rajoelina.
Kiongozi wa sasa wa Madagascar, Andry Nirina Rajoelina.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa Maneja wa Kituo hicho cha Radio Free FM, Lalatiana Rakotondrazafy, matangazo hayatarushwa mpaka hapo uongozi wa kituo hicho utakapokuwa na uhakika, pasi na shaka, kuwa hawatapokea vitisho vingine vya jeshi.

Akizungumza na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) leo hii (24. 07. 2012) Lalatiana amesema kwanza waliona askari wakiingia kituoni hapo asubuhi ya Jumapili, wakati ambapo uasi ndio ulikuwa ukianza katika kituo kimoja cha kijeshi, jirani na kiwanja cha ndege kikuu cha taifa hilo la kisiwa.

Baadhi ya vijana wakiandamana mjini Antananarivo.
Baadhi ya vijana wakiandamana mjini Antananarivo.Picha: picture-alliance/dpa

Jinsi Kituo cha Free FM kilivyoingiliwa

Kwa mshangao wa watangazaji studioni hapo, askari hao walikata umeme, na kukatisha mawimbi ya matangazo hayo kwa zaidi ya saa saba mfululizo.

Baada ya kumaliza kufanya walichokijia, meneja huyo wa radio ya wapinzani anasema askari hao wakakusanyika mtaani mbele ya jengo la kituo hicho. Lalatiana akawaambia watangazaji na wafanyakazi wengine kukusanya vyombo vyao vya kazi na kuondoka.

Wakati hayo yakiendelea, askari hao wakawanyangánya waandishi kompyuta na kifaa cha kurekebishia umeme yaani - voltage regulator.

Wakati wa uasi huo, Free FM ilitangaza sekeseke hilo na kurusha hewani sauti ya askari mmoja akikiri kwamba kuna mapinduzi yanaendelea Madagascar, taarifa iliyokemewa vikali na Wizara ya Mawasiliano ikidai kuwa itakichukulia chombo hicho hatua za kisheria.

Damu ilimwagika Jumapili iliyopita

Watu watatu, akiwemo kiongozi wa uasi huo, waliuwawa Jumapili hiyo wakati wa mapambano ya wanajeshi na askari hao katika kambi ya jeshi karibu na kiwanja cha ndege, mjini Antananarivo.

Tukio hilo limeshuhudiwa kabla ya kufanyika kwa mazungumzo katika Visiwa vya Ushelisheli, baina ya kiongozi wa sasa, Andry Rajoelina, na rais aliyengólewa kinguvu madarakani, Marc Ravalomanana, mwaka 2009 baada ya jeshi na maandamano kumpinga..

Raia wakishangaa muda mfupi baada ya mapinduzi mwaka 2009.
Raia wakishangaa muda mfupi baada ya mapinduzi mwaka 2009.Picha: AP

Jeshi ambalo, mara kwa mara, hujiingiza katika siasa nchini Madagascar, limechangia vikubwa kuinuka kwa Rajoelina, lakini mapinduzu hayo yamesababisha taifa hilo kutengwa na Jumuiya ya Kimataifa huku wafadhili wakiondoa misaada yao.

Mataifa ya Afrika pia yameifutia Madagascar uanachama katika jumuiya zakeWakati huo huo, Wizara ya Mambo ya nchi za Nje ya Ushelisheli, imesema Rais Ravalomanana amewasili kisiwani hapo jana na sasa yupo Desroches, kisiwa kilichopo umbali wa kilomita 230 kutoka katika eneo litakalofanyika mazungumzo ya upatanishi.

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ; ambayo ndio mpatanishi mkuu wa mgogoro huo wa Madagascar, inatarajia kuwakutanisha mahasimu hao wawili ana kwa ana hapo kesho (25.07.2012).

SADC imewapa muda Ravalomanana na Rajoelina mpaka tarehe 31, mwezi huu kuhakikisha wanamaliza tofauti zao.

Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman