Jeshi la Uturuki lashambulia tena waasi wa PKK.
23 Desemba 2007Ankara. Jeshi la Uturuki limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya maeneo ya waasi wa Kikurdi wanaotaka kujitenga walioko kaskazini mwa Iraq. Duru za Wakurdi wa Iraq zinasema kuwa ndehe za kivita za Uturuki zimeshambulia maeneo ya vijiji ambayo wakaazi wake wameondolewa kabla ya mashambulizi hayo na kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa. Hili ni shambulio la hivi karibuni kabisa miongoni mwa mashambulizi kadha yaliyolengwa kwa waasi wa PKK. Siku ya Jumanne kiasi cha wanajeshi 300 walivuka mpaka kwa muda na kuingia ndani ya Iraq na mwishoni mwa juma lililopita ndege za kijeshi zilishambulia maeneo ya waasi katika eneo hilo. Uturuki inadai kuwa waasi wa PKK wanatumia eneo la mpaka kati ya Iraq na Uturuki kama eneo la kujificha na kisha kufanya mashambulizi ndani ya Uturuki.