1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Umoja wa Mataifa kwa Lebanon?

Maja Dreyer19 Julai 2006

Wakati vita kati ya Israel na kundi la Hisbollah la nchini Lebanon vinazidi kuwa vikali, jumuiya ya kimataifa inafikiria vipi mapigano hayo yanaweza kusimamishwa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alipendekeza kupeleka jeshi maalum la kuweka amani kwenye mpaka kati ya nchi hizi mbili.

https://p.dw.com/p/CHLQ

Kwa mujibu wa wanadiplomasia, Umoja wa Mataifa unapanga kuongeza ujumbe wake wa amani uliopo mpakani mwa Israel na Lebanon, UNIFIL. Lengo ni kuweka eneo la usalama kati ya nchi hizi mbili. Katika hatua ya kwanza wanadiplomaisa hawa wanapanga kupendekeza jeshi la Lebanon liingie eneo la Kusini mwa nchi yao ili lisaidie kisimamisha mashambulizi ya Hisbollah.

Kabla ya mpango huu kuamuliwa, wanadiplomasia hawa wa kimataifa wanataka kuzungumza na viongozi wa Israel na Lebanon ili wapate makubaliano kutoka pande zote mbili kwa hatua hiyo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anataka ujumbe maalum ya kuweka amani nchini Lebanon uundwe kwa kuwa ujumbe wa UNIFIL wa wanajeshi 2000 hivi mpaka sasa hauna uwezo wa kusimamisha mapigano. Ujumbe huu mpya uwe mkubwa zaidi – idadi ya wanajeshi 10.000 ilitajwa – na uwe na uwezo mkubwa.

Alipofika mjini Bruxelles jana, Annan alisema: “Lazima baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likubali dhamana hiyo. Tayari katika azimio la zamani na Umoja wa Mataifa ilitakiwa, wapiganaji wote waliopo Kusini mwa Lebanon wavuliwe silaha zao. Hilo ni jukumu la serikali ya Lebanon.”

Annan anatarajiwa kesho kuongea mbele ya baraza la usalama. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleeza Rice, tayari alikubali pendekezo hili la Bw. Annan akisema bila ya jeshi la kimataifa haitawezekana kusimamisha mapigano. Waziri wa nje wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, pia alisema pendekezo hili ni hatua ya kwanza katika kutafuta amani.

Serikali ya Israel ina mashaka juu ya pendekezo hili la kupeleka kuongeza majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika eneo ya mpaka kati ya Lebanon na Israel. Ikiwa jeshi hili halitakuwa na uwezo wa kusimamisha mashambulizi ya makombora ya Hisbollah nchini Israel, hili si suluhisho litakalofaa, alisema naibu waziri mkuu wa Israel, Shimon Peres, akitaja ujumbe wa kijeshi Umoja wa Mataifa katika mpaka huo, UNIFIL, ambao tayari unafanya kazi huko tangu miaka ya 70 bila ya kuweza kuizuia Hisbollah kuishambulia Israel.