1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ukraine lavunja madaraja Urusi

18 Agosti 2024

Ukraine inasema imeliharibu daraja muhimu kwenye mkoa wa Kursk nchini Urusi na kulishambulia jengine la karibu na hapo, chini ya wiki mbili tangu ianze uvamizi wake ulioziharibu kabisa njia za kusambazia vifaa za Urusi.

https://p.dw.com/p/4jbDq
Picha ya jeshi la anga la Ukraine ikionesha daraja lililokatwa vipande viwili kwenye mkoa wa Kursk, Urusi.
Picha ya jeshi la anga la Ukraine ikionesha daraja lililokatwa vipande viwili kwenye mkoa wa Kursk, Urusi.Picha: Ukraine's Air Force Commander Mykola Oleshchuk via REUTERS

Wanablogu wanaoiunga mkono serikali ya Urusi wamethibitisha kuharibiwa kwa daraja la kwanza kwenye Mto Seim karibu na mji wa Glushkovo. 

Kwa mujibu wa wanablogu hao, hatua hiyo inaingilia moja kwa moja uwezo wa jeshi la Urusi kufikisha vifaa na bidhaa linazohitaji kukabiliana na uvamizi huu wa Ukraine. 

Hata hivyo, bado jeshi la Urusi linaweza kutumia vivuko na madaraja madogo madogo kwenye eneo hilo.

Mkuu wa jeshi la anga la Ukraine, Luteni Mykola Oleshchuk, alichapisha siku ya Ijumaa (Agosti 16)  video ya mashambulizi ya anga yaliyolisambaratisha daraja hilo vipande viwili. 

Soma zaidi: Zelenskyy asema vikosi vya Ukraine vimeukamata mji wa Urusi

Chini ya siku mbili baada ya hapo, vikosi vya jeshi la Ukraine vililishambulia daraja jengine nchini Urusi, kwa mujibu wa Oleshchuk na gavana wa jimbo hilo, Alexei Smirnov.

Kufikia asubuhi ya Jumapili (Agosti 18), hakukuwa na taarifa yoyote rasmi juu ya hasa lilipo daraja la pili lililoshambuliwa. 

Chaneli za mtandao wa Telegram zilidai kwamba daraja hilo lilikuwa kwenye kijiji cha Zvannoe kando kidogo ya mji wa Seim.

Kwa mujibu wa mtandao wa Mash nchini Urusi, mashambulizi hayo yamelibakishia eneo hilo daraja moja tu kwa sasa. 

Jeshi la Urusi lakatiwa njia za usambazaji

Shirika la habari la AP halikuweza kuthibitisha madai hayo mara moja, lakini endapo yakithibitishwa, basi mashambulizi ya Ukraine yatakuwa yanazidi kurejesha nyuma juhudi za vikosi vya Urusi kuukomboa mkoa wa Kurskna kuwahamisha raia.

Picha ya jeshi la anga la Ukraine ikionesha daraja lililokatwa vipande viwili kwenye mkoa wa Kursk, Urusi.
Picha ya jeshi la anga la Ukraine ikionesha daraja lililokatwa vipande viwili kwenye mkoa wa Kursk, Urusi.Picha: Mykola Oleshchuki/via REUTERS

Mji wa Glushkovo upo umbali wa kilomita 12 kaskazini mwa mpaka wa Ukraine na takribani kilomita 16 kaskazini magharibi kutoka eneo la mapigano la Kursk. Zvannoe iko umbali wa kilomita 8 upande wa kaskazini mashariki..

Soma zaidi:Ukraine yakanusha kuhusika kulipua bomba la Nord Stream 2

Kyiv imekuwa haisemi mengi kuhusu mipango na malengo ya uvamizi wake huu wa kushtukizia, yakiwa mashambulizi ya kwanza makubwa kabisa dhidi ya Urusi tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, na ambayo yaliishangaza Kremlin na kushuhudia vijiji kadhaa na mamia ya wafungwa wakiangukia mikononi mwa Ukraine.

Jeshi la Ukraine limeingia ndani kabisa ya mkoa wa Kursk wakipitia maeneo mbalimbali, huku wakikumbana na upinzani mdogo kabisa na kusababisha mtafaruku na fadhaa miongoni mwa raia.

Kamanda wa jeshi la Ukraine, Jenerali Oleksandr Syrskyi, alidai wiki iliyopita kwamba vikosi vyake sasa vinadhibiti eneo lenye ukubwa wa kilomita 1,000 za mraba ndani ya mkoa wa Kursk.

Chanzo: AP