Jeshi la Syria laukomboa mji wa Aleppo
23 Desemba 2016Wakati vikosi vya jeshi la Syria vikiudhibiti kikamilifu mji wa Aleppo mashambulizi ya kutokea angani yaliyofanywa na Uturuki yamewaua karibu raia 47 wakiwemo watoto 14. Sylvia Mwehozi anayo taarifa zaidi.
Tangazo hilo limekuja baada ya mpango wa kihistoria wa uokoaji raia uliofikisha kikomo mashambulizi ya muda mrefu mashariki mwa Aleppo yaliyokuwa yakitekelezwa na vikosi vya serikali pamoja na washirika wake.
Maelfu ya wakazi katika maeneo ya magharibi mwa mji huo ambao umesalia katika udhibiti wa serikali katika kipindi chote cha mgogoro, waliingia mitaani, wakiimba na kushangilia licha ya kuwepo na baridi kali kama anavyosema mmoja wa wakazi wa eneo hilo, "tuna kila sababu ya kusherehekea. Ushindi huu wa Aleppo ni mkubwa na Inshallah tutawaondoa magaidi kote nchini Syria. Nina imani Aleppo ni mwanzo na mwisho wa kila kitu na naamini Mungu atawaondoa magaidi wote nchini Syria."
Taarifa ya jeshi imetangaza kurejea kwa usalama Aleppo baada ya kuondolewa kwa magaidi na kuondoka kwa wale waliosalia pale.
Afisa mmoja wa kundi la waasi la Nureddin al-Zinki, Yasser al-Youssef amesema hilo ni pigo kubwa kwa mapinduzi dhidi ya rais Bashar al-Assad. Nikimnukuu anasema "katika ngazi ya kisiasa, hili ni pigo kubwa."
Tangazo la jeshi limekuja baada ya televisheni ya taifa kusema msafara wa mwisho wa mabasi manne yaliyokuwa yamewabeba waasi na raia kuondoka mashariki mwa Aleppo na kuwasili katika wilaya ya Ramusa inayoshikiliwa na serikali kusini mwa mji huo.
Mapema, shirika la msalaba mwekundu lilitoa taarifa kuwa zaidi ya wapiganaji 4000 wameondoka katika maeneo ya waasi katika hatua za mwisho za zoezi la kuwahamisha.
Kabla ya tangazo hilo Rais Bashar al-Assad amenukuliwa na shirika la habari la taifa, SANA akisema kuwa "ukombozi wa Aleppo si ushindi tu kwa Syria bali pia kwa wale waliochangia mapambano dhidi ya magaidi, hususan Urusi na Iran".
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alitangaza jana mashambulizi ya anga yaliwaua jumla ya wapiganaji 35,000 tangu ilipoingilia kati mgogoro huo.
Uturuki nayo ilianzisha kampeni yake mwishoni mwa mwezi Agosti ikiwaunga mkono waasi wa Ankara, kwa lengo la kuwakimbiza wapiganaji wa Dola la Kiislamu pamoja na wapiganaji wa Kikurdi karibu na mpaka wake.
Hapo jana alhamis IS ilitoa mkanda wa vidio wa dakika 19 ukiwaonesha askari wawili wa Uturuki wakichomwa hai, hiyo ikiwa ni baada ya Uturuki kuapa kupambana na "ugaidi" nchini Syria na kulipa kisasi kwa wapiganaji wake 16 waliouliwa.
Wakati hayo yakijiri mashambulizi ya anga ya Uturuki yamewaua karibu raia 47 wakiwemo watoto 14 katika mji unaoshikiliwa na IS wa Al-Bab ambao vikosi vya Uturuki vimekuwa kwa wiki kadhaa vikipigania kuudhibiti.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Josephat Charo