1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Syria laigawa Ghouta Mashariki

10 Machi 2018

Vikosi vya serikali ya Syria vimeugawa mji wa Douma, ambao ni mkubwa katika ngome inayoshikiliwa na waasi Ghouta Mashariki kutoka kwenye eneo jengine lililobakia la mji huo.

https://p.dw.com/p/2u5pU
Syrien Angriffe auf Ost-Ghuta
Picha: Reuters/B. Khabieh

Jeshi la Syria leo limedhibiti zaidi ya nusu ya Ghouta Mashariki kutokana na mashambulizi ya wiki tatu, ikiwemo barabara inayoiunganisha miji ya Douma na Harasta miji miwili mikubwa Ghouta Mashariki na kuligawa eneo hilo katika sehemu tatu, huku Douma ikiwekwa na maeneo yanayouzingira, Harasta ukiwa upande wa magharibi na maeneo yaliyobaki yakielekezwa upande wa kusini.

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema kuwa jeshi la Syria pia limeudhibiti mji wa Misraba wakati likisonga mbele, huku barabara kati ya Douma na Harasta zikiwa ndani ya eneo ambalo mashambulizi yanaweza kufanywa.

Shirika la habari la Ufaransa, AFP limeripoti kuwa mashambulizi ya anga pamoja na makombora yamekuwa yakiendelea leo Jumamosi. Makundi mawili makuu ya waasi wenye itikadi kali za Kiislamu ya Jaish al-Islam na Failaq al-Rahman bado yamebakia Ghouta Mashariki, pamoja na idadi ndogo ya wapiganaji kutoka kundi la Nusra Front ambalo lilikuwa tawi la mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda nchini Syria.

Syrien Krieg - Ostghuta bei Damaskus | Kinder
Watoto wakiwa Ghouta MasharikiPicha: Reuters/B. Khabieh

Februari 18, majeshi ya serikali yalianzisha mashambulizi Ghouta Mashariki, eneo la mwisho linalodhibitiwa na waasi karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus na sasa yanaudhibiti zaidi ya nusu ya mji huo. Kwa mujibu wa shirika hilo, mashambulizi hayo yamesababisha raia wapatao 1,000 kuuawa, zaidi ya robo ya idadi hiyo wakiwa watoto. Mamia ya watu wamejeruhiwa.

Zaidi ya watu 400,000 wamezingirwa

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kiasi ya watu 400,000 wamezingirwa katika eneo hilo ambalo limekuwa chini ya udhibiti wa waasi tangu 2013. Licha ya Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kusitishwa kwa muda mapigano nchini Syria, serikali ya Rais Bashar al-Assad imeendelea na operesheni yake kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji wenye itikadi kali kwenye eneo hilo.

Wakati huo huo, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan leo ameahidi kuongeza mashambulizi ya Uturuki nchini Syria dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi hadi kwenye miji muhimu ya mpakani inayodhibitiwa na wanamgambo hao hadi kwenye eneo la mpaka na Iraq.

Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria, vikosi vya Uturuki vimesonga mbele na kufika kwenye viunga vya mji wa Afrin baada ya operesheni ya wiki kadhaa dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria, YPG. Uturuki na makundi washirika ya waasi yanasonga mbele kwenye mji huo kutoka mashariki huku vikifanya mashambulizi ya mabomu.

Syrien CIRC-Hilfskonvoi in der belagerten Stadt Douma
Msafara wa ICRC katika mji wa DoumaPicha: Reuters/B. Khabieh

Januari 20, mwaka huu Uturuki ilianzisha operesheni yake ya kuwaondoa wapiganaji wa YPG, kutoka mji wa Afrin ulioko kaskazini mwa Syria.

Jana usiku idadi ndogo ya wapiganaji wa Nusra Front waliruhusiwa kuondoka Ghouta Mashariki na familia zao chini ya mkataba maalum. Aidha, Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu duniani, ICRC iliripoti kuwa malori 13 yaliyojaa msaada wa kuwafikia kiasi ya watu 12,000 Ghouta Mashariki, kabla ya kulazimika kuondoka baada ya kuanza tena kwa mashambulizi.

Mwandishi: Grace Patrcia Kabogo/AP, DPA, AFP, Reuters, DW http://bit.ly/2FnB6YN
Mhariri: Isaac Gamba