1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la pamoja Afrika Mashariki kuanza kazi Desemba

Admin.WagnerD21 Agosti 2014

Nchi kumi za ukanda wa mashariki mwa bara la Afrika zimekubaliana kuunda kikosi cha pamoja cha askari jeshi na polisi ambacho kitakuwa tayari kuingilia kati mahali popote miongoni mwa nchi hizo ifikapo mwezi Desemba.

https://p.dw.com/p/1Cyek
Eastern Africa Standby Force
Picha: DW/L. Ndinda

Azimio hilo lilitangazwa na wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi hizo kwenye kikao chao kilichofanyika mjini Kigali Rwanda.Uamuzi huo ni jitihada za kukabiliana na visa vya ukosefu wa usalama vinavyosababishwa na makundi ya ugaidi yanayopatikana kwenye ukanda huo wa Afrika mashariki.

Uamuzi wa kuwepo kwa kikosi imara cha kukabiliana na mizozo uliazimiwa na umoja wa Afrika ili kwamba ifikapo mwezi wa kumi na mbili hapo mwaka ujao kuwepo na vikosi vya aina hii kutoka kanda tano za bara la Afrika ikiwemo kanda ya Afrika mashariki.

Hata hivyo kutokana na tatizo la usalama mdogo unaosababishwa na makundi ya kigaidi katika kanda ya mashariki mwa Afrika viongozi wa nchi hizo kumi walikubaliana mwezi Juni mwaka huu kwenye kikao chao kilichofanyika nchini Equatorial Guinea kwamba ni lazima kuundwe kikosi jumla cha jeshi kabla ya kumalizika mwezi Desemba mwaka huu.

Wanajeshi wa kikosi cha pamoja wakiwa mazoezini huko nyuma.
Wanajeshi wa kikosi cha pamoja wakiwa mazoezini huko nyuma.Picha: DW/L. Ndinda

Maandalizi ya miaka kumi

Sasa wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi hizo wamepitisha kwa kauli moja kuanzishwa kwa kikosi hicho. "Tulianza mwaka 2004 na leo ni mwaka 2014, kwa hiyo kwa mika kumi tulikuwa tunatoa mafunzokwa wale watakaojiunga na kikosi hicho, na tunaona tumefanya maandalizi ya kutosha kuweza kuanza mwezi Desemba," alisema Brigedia Jenerali Tai Gitwai kutoka secretariati ya mataifa hayo.

Naye msemaji wa jeshi la Rwanda Brigedia Joseph Nzabamwitu, alipoulizwa namna kikosi hicho kitakapoingilia katika nchi inayokabiliwa na changamoto za kiusalama wakati kila nchi ina mamlaka yake, alisema nchi zilizounda kikosi hicho zinaelewana, na hivyo watakaa na kukubaliana juu ya tatizo linalotokea mahali fulani. "Kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kukaa na kutathmini hali ya mambo kabla ya kuchukua maamuziktk ngazi mbalimbali," alifafanua Jenrarali huyo.

Mapendekezo ya wakuu hao wa majeshi kuhusiana na kuundwa kwa kikosi hicho yalikuwa yanajadiliwa na mawaziri wenye dhama ya ulinzi katika mataifa husika, ambao walitarajiwa kuyaidhinisha na kutangaza idadi kamili ya askari watakaounda kikosi hicho.

Mwandishi: Sylivanus Karemera

Mhariri: Josephat Charo