1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Myanmar layachoma makazi ya Warohingya

Caro Robi
18 Desemba 2017

Shirika la kuteteta haki za binadamu, Human Rights Watch, limesema Jeshi la Myanmar lilizichoma moto nyumba za Warohingya siku chache baada ya Myanmar kusaini makubaliano na Bangladesh ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi.

https://p.dw.com/p/2pYZq
Myanmar Luftaufnahme eines verbrannten Rohingya Dorfes in der Nähe von Maungdaw
Picha: Reuters/S. Z. Tun

Shirika la kimataifa la kuteteta haki za binadamu, Human Rights Watch, limesema jeshi la Myanmar lilizichoma moto nyumba kadhaa za Warohingya siku chache baada ya Myanmar kusaini makubaliano na Bangladesh ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi, hiyo ikimaanisha makubaliano hayo yalikuwa tu ya kuhadaa umma.

Human Rights Watch inasema kutokana na picha za satelaiti walizozikusanya, makazi ya Warohingya katika vijiji 40 yalichomwa moto mwezi Oktoba na Novemba na hivyo kuongeza idadi ya vijiji vilivyochomwa moto tangu mwezi Agosti kufika 354.

Ripoti ya shirika hilo imesema majengo kadhaa yalichomwa moto wiki ambayo Myanmar ilitia saini makubaliano na nchi jirani ya Bangladesh ambako Warohingya wamekimbilia. Makubaliano hayo yaliyofikiwa tarehe 23 mwezi uliopita yanasema wakimbizi watarejeshwa Myanmar katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

HRW: Myanmar haina nia ya kuushughulikia mzozo wa Rohingya

Brad Adams, mkurugenzi wa Human Rights barani Asia amesema kitendo hicho cha Jeshi kuvichoma vijiji vya Warohingya, jamii ya Waislamu walio wachache nchini humo inaonesha wazi kuwa Myanmar haijajitolea kwa dhati kuutatua mzozo wa Rohingya na usalama wa wakimbizi ni suala linalopaswa kuzingatiwa kwa uzito.

Rohingya-Flüchtlinge in Bangladesch
Warohingya wakielekea Bangladesh wakikimbia ghasia MyanmarPicha: picture-alliance/dpa/Zumawire/Km Asad

Zaidi ya Warohingya laki sita wamekimbilia Bangladesh tangu mwezi Agosti baada ya kuzuka ghasia katika jimbo la Rakhine. Umoja wa Mataifa na Marekani zimeyataja mateso dhidi ya Warohingya yanayolenga kuwaangamza jamii moja.

Mkuu wa tume ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al Hussein, amesema ghasia dhidi ya Warohingya ina ishara za kuwa mauaji ya halaiki.

Al Hussein ameliambia shirika la Habari la BBC kuwa mashambulizi dhidi ya Warohingya yalipangwa vilivyo na kumtaka  kiongozi wa Myanmar Aung Suu Kyi kuchukua hatua zaidi kukomesha operesheni ya kijeshi dhidi ya Warohingya.

Mkuu huyo wa tume ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema hatashangaa siku moja katika siku za usoni mahakama ikaamua kuwa kulikuwa na vitendo vya mauaji ya halaiki dhidi ya Warohingya, jamii ya Waislamu walio wachache nchini Myanmar. Serikali ya Myanmar imekanusha madai kuwa imewalenga Warohingya.

Phil Robertson, naibu wa mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch barani Asia amesema Myanmar inacheza mchezo wa danganya toto, huku kiongozi wa Myanmar, Aung Suu Kyi, na kundi lake wakitia saini makubaliano ya kuwarejesha Warohingya wakifahamu fika kuwa hakuna hakikisho kuwa watakaorejea watakuwa salama hasa kwa misingi kuwa vikosi vya usalama vinaendeleza operesheni ya kuvichoma vijiji ambavyo Warohingya wanapaswa kurejea kuishi.

Mashirika ya kutoa misaada yamesema yatasusia mipango ya kuundwa kwa kambi mpya za wakimbizi katika jimbo la Rakhine. Wiki iliyopita, shirika la madaktari wasio na mipaka MSF walitoa takwimu kuwa tariban Warohingya 7,000 wameuawa katika ghasia zinazojiri Rakhine tangu mwezi Agosti.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/Dpa

Mhariri: Mohammed Khelef