Jeshi la Mali lawaachilia rais na waziri mkuu waliojiuzulu
27 Mei 2021
Kwa mujibu wa msemaji wa kamanda huyo wa kijeshi aliyechukuwa madara, kuachiliwa huru kwa rais N'Daw na waziri mkuu Ouane, kunakuja baada ya kujiuzulu kwao hapo jana mbele ya wapatanishi wa kimataifa walioko katika taifa hilo kusulushisha mzozo wa kisiasa uliopo.
Msemaji huyo, Baba Cisse ameongeza kwamba watu wanapaswa kujuwa kwamba makamu wa rais wa mpito alifanya kila kitu katika uwezo wake kuhakikisha kuwa hali haifikii jinsi ilivyo sasa.
Ameongeza kwamba kama mwanajeshi, angeweza kuthibitisha tu nafasi yake kama mdhamini wa uthibiti na kulitetea taifa.
Umoja wa Mataifa wasema kujiuzulu kulikuwa kwa kulazimishwa
Baada ya mkutano wa faragha hapo jana, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lilisema kuwa hatua ya kujiuzulu ilikuwa ya kulazimishwa na kutaka kurejelewa tena mara moja kwa kipindi cha mpito kinachoongozwa na raia na kusema kuwa jeshi linapaswa kubakia kambini.
Umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa pamoja na Marekani, pia yalilihimiza jeshi la Mali kuwaachia huru viongozi hao wa mpito.
Kujiuzulu kwao kunasadifiana na ziara ya ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS nchini humo kushinikiza jeshi la nchi hiyo kujiondoa. Jumuiya hiyo ya ECOWAS imeelezea uwezekano wa vikwazo dhidi ya maafisa waliohusika katika hatua hizi za hivi karibuni.
Athari ya kukamtwa kwa viongozi hao
Kukamatwa kwa viongozi hao kulikopangwa na naibu rais Assimi Goita, kumetatiza kurejea kwa Mali katika demokrasia baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Agosti mwaka jana yaliomuondoa madarakani rais Ibrahim Boubacar Keita.
Goita, ambaye ni kanali, aliongoza mapinduzi hayo ya mwaka jana. Alikuwa ameahidi kwamba uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaja ujao utaendelea kulingana na ratiba. Cisse ameliambia shirika la habari la reuters kwamba habari kuwahusu Ndaw na Ouane zitawekwa siri kwa ajili ya usalama wao. Alikataa kuelezea mipango yoyote ya kujaza nafasi zao
N'Daw na Ouane walikamatwa siku ya Jumatatu pamoja na viongozi wengine wa serikali ya mpito, saa chache baada ya kulitangaza baraza jipya la mawaziri ambalo halikuwajumuisha viongozi wawili wakuu wa jeshi.
Kwa kuondolewa kwa viongozi hao wawili wa mpito, kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Mali ya mwaka 2020 kanali Assimi Goita ambaye amekuwa akihudumu kama makamu wa rais wa mpito tangu mwezi Septemba, amechukuwa udhibiti wa taifa hilo la Afrika Magharibi.