1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Jeshi la Israel laondoka katika hospitali ya Al-Shifa Gaza

Hawa Bihoga
1 Aprili 2024

Jeshi la Israel IDF limeondoka katika hospitali ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza leo baada ya wiki mbili za oparesheni kali ya kijeshi katika hospitali hiyo.

https://p.dw.com/p/4eJMy
Jengo la hospitali ya Al-Shifa
Jengo la hospitali ya Al-ShifaPicha: AFP

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hapo jana Jumapili aliitaja oparesheni ya kijeshi katika hospitali al-shifa kuwa ni ya mafanikio makubwa na kuongeza kwamba "zaidi ya magaidi 200 wameuwawa na wengine mamia walijisalimisha."

Kwa mujibu wa Israel, kundi la Hamas kwa mara nyingine tena limeweka vituo vya kuongoza mashambulizi katika maeneo mengi baada ya Israel kuivamia hospitali ya Al-shifa mnamo mwezi Novemba.

Soma pia: ICJ yataka Israel kuruhusu misaada zaidi kuingia Gaza

Mara kadhaa Israel imekuwa ikiishutumu Hamas kwa kutumia vibaya vituo vya matibabu kwa madhumuni ya kijeshi. Hatua ambayo inakanushwa vikali na Hamas.

Juma lililopita msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alisema kuwa Hamas pamoja na wapiganaji wengine walikuwa wakijihifadhi katika hospitali hiyo na kwamba walijibu mashambulizi kutokea chumba cha dharura pamoja na wodi ya wazazi.