JERUSALEM: Wanajeshi wa Israel wavuka mpaka na kuingia Lebanon
19 Julai 2006Wanajeshi wa Israel leo asubuhi wamevuka mpaka na kuingia eneo la kusini mwa Lebanon kufanya mashambulio dhidi ya ngome za wanamgambo wa kundi la Hezbollah.
Msemaji wa jeshi ameieleza operesheni ya sasa kuwa yenye mipaka na inayolenga maeneo maalumu. Ameongeza kuwa wanajeshi hao wameingia Lebanon lakini wataondoka wakati watakapomaliza kazi yao ya kuwachakaza wanamgambo wa Hezbollah katika eneo la mpakani na kuzuia shehena za silaha kuwafikia kutoka Syria.
Jenerali Alon Friedman wa jeshi la Israel ameiambia redio ya jeshi nchini Israel kwamba wamefaulu kuharibu asilimia 50 ya silaha za Hezbollah.
Akizungumza kuhuzu mapigano haya rais George W Bush wa Marekani amesema, ´Kila mtu anahuzunishwa na kuuwawa kwa watu wasio na hatia. Lakini kwa upande mwingine tunachotambua ni kwamba sababu kubwa ya tatizo hili hi Hezbollah na tatizo hili lazima litafutiwe ufumbuzi.´
Wanamgambo wa Hezbollah wamevurumisha maroketi katika mji wa bandari wa Haifa nchini Israel. Jengo moja limeharibiwa lakini hakuna ripoti za majerauhi zilizotolewa.
Hapo awali ndege za Israel zilishambulia maeneo yaliyo karibu na uwanja wa ndege wa Beirut na kusini mwa Lebanon usiku wa nane mfululizo wa mashambulio ya jeshi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon.
Ndege za Israel pia zimeiharibu dajara moja katika mji wa kusini wa Sidon nchini Lebanon.