1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Wanajeshi wa Israel waanza kuondoka Lebanon

14 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDLh

Wanajeshi wa Israel wameanza kuondoka kutoka eneo la kusini mwa Lebanon mapema leo. Hatua hii inafuatia kuanza kutekelezwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa lililonuia kumaliza vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema jeshi litaliheshimu azimio hilo lakini litaendelea kuwa na haki ya kujilinda na kuwalinda raia wa Israel. Viongozi wa ngazi ya juu nchini Israel wamekubali kuondoka kwa wanajeshi wao kutoka Lebanon, lakini wamesema wanajeshi wataendelea kubakia katika baadhi ya maeneo muhimu mpaka yatakapokabidhiwa kwa jeshi la Lebanon na kikosi cha Umoja wa Mataifa.

Azimio la Umoja wa Mataifa linataka mapigano yakomeshwe na wanajeshi elfu 15 wa Umoja wa Mataifa wapelekwe Lebanon. Linataka pia wanajeshi elfu 15 wa Lebanon wachukue nafasi ya wanamgambo wa Hezbollah watakaopokonywa silaha kusini mwa Lebanon. Israel inatakiwa iwaondoe wanajeshi wake wote elfu 30 kusini mwa Lebanon.

Akizungumza juu ya azimio la Umoja wa Mataifa, waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni amesema, ´Sasa huu ni wakati wa mtihani, sio tu kwa serikali ya Lebanon, lakini kwa jamii ya kimataifa. Tunatarajia jamii ya kimataifa kulitekeleza azimio hili na jambo hili likifanyika haraka itakuwa vizuri zaidi.´

Mashambulio yaliendelea usiku kucha hadi wakati wa kuanza kutekelezwa azimio la Umoja wa Mataifa. Wanajeshi wa Israel waliushambulia mji wa Sidon na kukabiliana na wanamgambo wa Hezbollah katika mapigano makali.

Pande zote mbili zimesema zitafanya mashambulio ikiwa azimio hilo halitaheshimiwa.

Habari za hivi punde zinasema wanajeshi wa Israel wamemuua mwanangambo mmoja wa Hezbollah alipokikaribia kikosi chao katika hali ya kutisha. Israel imesema kuuwawa kwa mwanamgambo huyo sio ukiukaji wa azimio la Umoja wa Mataifa.