JERUSALEM: Mapigano yaendelea nchini Lebanon
1 Agosti 2006Mapambano makali yamezuka kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon mapema leo Jumanne.Duru za kijeshi za Israel zimesema mapigano yamezuka katika eneo la Aita al-Shaab na Taibe ndani ya ardhi ya Lebanon.Wanamgambo wa Hezbollah wamesema wanapambana vile vile na kikosi kingine cha Kiisraeli karibu na kijiji cha mpakani cha Kfar Kila.Hapo awali jeshi la Israel lilipewa idhini ya kupanua mashambulio yake ndani ya Lebanon.Operesheni hiyo itawaingiza Lebanon ndani zaidi kuliko hivi sasa.Radio ya Israel imesema,operesheni hiyo huenda ikawajumuisha wanajeshi wengine wa akiba wapatao elfu 15.Kwa mujibu wa duru za kisiasa nchini Israel,lengo la jeshi ni kuwasukuma nyuma wanamgambo wa Hezbollah,kama kilomita 20 kaskazini ya mpaka, ili vikosi vya kimataifa viweze kupelekwa katika eneo hilo.Wakati huo huo,wanadiplomasia mjini Brussels wamesema,mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya watakutana leo Jumanne kujadili uwezekano wa kusitisha mapigano na kupeleka misaada ya kiutu nchini Lebanon.