1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Mapigano yaendelea Lebanon

1 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDPr

Ndege za Israel zimevishambulia vijiji vya Washia kusini mwa Lebanon hii leo. Ngome za wanamgambo wa kundi la Hezbollah ndani ya maeneo ya Lebanon na maeneo mengine yanayokaliwa na raia kwenye pwani ya bahari ya Mediterenia pia yameshambuliwa.

Wanamgambo wa Hezbollah wanaendelea kukabiliana na wanajeshi wa Israel katika mapigano makali kwenye maeneo ya Taibe, Adaisseh na Kfaf Kila, karibu na mpaka wa Lebanon.

Wakati huo huo, kundi la Hezbollah limetangaza katika runinga yake ya Al Manar, kwamba limewaua wanajeshi watatu wa Israel katika kijiji cha mpakani cha Aita al Shaab. Kundi hilo limesema wapiganaji wake wanne wameuwawa kwenye mapigano hayo.

Wakati haya yakiarifiwa, bomu lililotengenezwa nchini Syria limetungiliwa karibu na barabara inayotumiwa na wanajeshi wa Israel wa kulinda usalama katika milima ya Golan. Duru za jeshi la Israel zinasema hakuna aliyejeruhiwa katika kisa hicho.

Habari kutoka Syria zinasema kikundi kinachopinga kukaliwa kwa maeneo ya Golan kililitega bomu hilo. Na habari kutoka Dubai zinasema kundi la wanawake wa Saudi Arabia leo wameitaka jumuiya ya kimataifa kusitisha mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel nchini Lebanon na katika Ukanda wa Gaza.

Makundi ya kiislamu ya kutoa misaada nayo yamekutana mjini Istanbul nchini Uturuki kujadili jinsi yatakavyoshirikiana kupeleka misaada nchini Lebanon na Palestina.