1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Mapigano yaendelea kusini mwa Lebanon

19 Julai 2006
https://p.dw.com/p/CG60

Wanajeshi wa Israel wanaendelea kukabilia na wanamgambo wa kundi la Hezbollah kusini mwa Lebanon, siku ya nane mfululizo. Watu takriban 57 na mwanamgambo mmoja wa Hezbollah wameuwawa. Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake watatu wameuwawa na wengine 10 wakajeruhiwa katika mapigano hayo.

Ndege za kivita za jeshi la Israel zimefanya mashambulio dhidi ya ngome za Hezbollah na kuziharibu kabisa nyumba takriban 20.

Wanamgambo wa Hezbollah wamejibu mashambulio hayo kwa kuvurumisha makombora katika mji wa Haifa, kaskazini mwa Israel.

Wakati huo huo, mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia sera za kigeni, Javier Solana, amesafiri kwenda Israel baada ya kukutana na maofisa wa ngazi ya juu mjini Beirut.

Akizungumza juu ya mapigano hayo, Solana amesema, ´Walio na uwezo na ushawishi wa kuyazuia machafuko haya wawajibike na wafanye hivyo mara moja. ´

Baada ya kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni, Solana ameyalaani mashambulio ya mpakani yanayofanywa na Hezbollah yaliyosababisha operesheni ya kijeshi ya Israel nchini Lebanon, lakini akasema juhudi za kidiplomasia za kuutanzua mgogoro huo zinatakiwa ziendelee.

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema mashambulio yataendelea mpaka wanajeshi wa Israel waachiliwe huru na kundi la Hezbollah lipokonywe silaha.