Je,raia kupunguziwa kodi kutasaidia kufufua uchumi?
24 Novemba 2008Basi tunaanza na gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG.Linasema:
Ukweli ni kuwa hadi hivi sasa hakuna anaejua kwa umbali gani mgogoro wa fedha wa hivi sasa utakavyoathiri uchumi duniani.Lakini tayari umma umekumbwa na hofu ya kutoweza kufanya cho chote kujikinga dhidi ya athari za mgogoro ulioikumba dunia nzima.
Likiendelea linasema,serikali kwa hivyo isizidi kuchochea hofu za umma Kwani wakati huu wa wasiwasi,wanasiasa hawawajibiki tu kuieleza hali halisi bali ni wajibu wao pia kurejesha imani iliyopotea,kutafuta suluhisho na muhimu zaidi ni kuwapa raia matumaini licha ya hali ngumu ya hivi sasa.Kwa hivyo linauliza Kansela Angela Merkel alidhamiria nini alipoonya juu ya hali mbaya ya uchumi itakayoendelea mwakani?
Lakini sasa tutupie jicho gazeti la NEUE PRESSE kutoka Hannover linaloeleza hivi: Kwa kuutazama ukweli kuwa mwakani serikali itakuwa na deni jipya la Euro bilioni 18,haiingi akilini kupunguza kodi.Kwani lengo muhimu ni kuwa na urari wa bajeti.Lakini muhimu zaidi ni kudhibiti mgogoro wa uchumi. Kwani wataalamu wameshaonya kuwa uchumi utadorora kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu miongo kadhaa.Labda kinyume na Ujerumani,Marekani na Uingereza zimetambua kwa kiwango gani uchumi wao utaathirika kwa hivyo zinatazamia kupunguza kodi ili raia wawe na pesa zaidi mifukoni.Serikali ya Ujerumani tangu mwanzoni inajaribu kutuliza hali.Itachangamka kuchukua hatua itakaposhindwa kuficha ukweli pale maafa yatakapotokea.
Gazeti la VOLKSSTIMME kutoka Magdeburg likiendelea na mada hiyo hiyo linaeleza hivi: Uingereza inataka kupunguza kodi ya ongezeko la thamani ya bidhaa VAT hatua itakayoleta faida zinazoeleweka kwa urahisi na kuwapa raia matumaini wakati ambapo benki zinakabiliwa na mizozo na wananchi hufikiria mara mbili kabla ya kutoa pesa zao.Kwa maoni ya gazeti hilo serikali itaweza kuongeza upya kodi hiyo mgogoro wa fedha utakapodhibitiwa na hivyo tena kuanza kukusanya fedha za kusawazisha madeni yake. Sasa nchini Ujerumani Kansela Angela Merkel ndio anazidi kushinikizwa kupunguza kodi.
Tunamalizia kwa uchambuzi wa gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linalosema: Rais mteule wa Marekani Obama katika kuchagua wale watakaoshiriki katika serikali yake atakaposhika madaraka mwakani, amedhihirisha kuwa ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi hazikuwa porojo za kampeni tu.Alimaanisha kweli kuleta mageuzi.Na huo ni mwanzo mzuri.