1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali Sejusa atupwa rumande

Emmanuel Lubega2 Februari 2016

Katika kile wengine wanachosema ni hila za kisasia za Rais Yoweri Museveni kupandikiza hofu miongoni mwa wapinzani wake, Jenerali Sejusa alisomewa mashitaka matano yanayohusu ushiriki wake katika kampeni.

https://p.dw.com/p/1HoBv
Picha: Getty Images/AFP/R. Sullivan

Jenerali Sejusa alifikishwa kwenye maeneo ya mahakama ya kijeshi ya Makindye saa 4:45 asubuhi na dakika 40 baadaye alisimamishwa kizimbani kusomewa mashtaka na mwenyekiti wa mahakama hiyo, Meja Jenerali Levi Karuhanga.

Shtaka la kwanza lililoleta mabishano ya akili kati ya mawakili wa pande zote mbili lilikuwa kitendo cha mkuu huyo wa zamani wa ujasusi kutoroka kutoka kazini mwaka 2013, huku mawakili wake wakilipinga vikali wakisema "Sejusa aliwasislisha shauri katika mahakama kuu akitaka kuruhusuiwa astaafu kutoka jeshi la UPDF na kwa kuwa maamuzi hayajafanywa, basi hastahili kufunguliwa mashtaka yoyote katika mahakama ya kijeshi."

Baada ya mabishano yaliyodumu kwa takribani saa moja na nusu, mwenyekiti wa mahakama aliendelea kusoma mashtaka mengine, likiwemo la uhusika wa jenerali huyo katika kampeni za kisiasa katika sehemu mbali mbali na kwenye makao makuu ya vyama vya kisiasa.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Hoshiko

Sejusa alaani kutendewa vibaya rumande

Alipopata nafasi, Jenerali Sejusa alisimulia masaibu yake ya siku tatu tangu alipokamatwa na kuzuiliwa katika korokoro ambamo Marehemu Iddi Amin ulimzuilia yeye akisubiri kifo. Akaongezea kwamba hakutaraji utawala wa Museveni kumdhalilisha jinsi hiyo ukimnyima haki zake za kibinadamu.

Juhudi za mawakali wake kuitaka mahakama hiyo imwachilie kwa dhamana ziliambulia patupu na badala yake alirejeshwa rumande hadi tarehe 9 Februari.

Kwa mtazamo wa baadhi ya watu kama vile Yosia Kasirye aliyekuwa miongoni mwa jamaa na marafiki waliofurika kweye mahakama hiyo, "mashataka dhidi ya jenerali huyo yanalenga kupelekea vitisho na hofu miongoni mwa wananchi ili wamchague Rais Museveni kwa awamu nyingine."

Wakati huo huo, serikali ya Rwanda imekanusha vikali madai yaliyotolewa na Jenerali Sejusa hivi majuzi kwamba ndege iliyosheheni karatasi za kura kwa uchaguzi wa Uganda, ilitua Kigali na kuacha sehemu fulani ya karatasi hizo ili zitumiwe kumsaidia Rais Museveni kwenye wizi wa kura.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Saumu Yusuf