Jean Ping azungumzia Uharamia pwani ya Somalia
20 Novemba 2008Rais wa halmashauri kuu ya umoja wa Afrika Jean Ping amesema kuwa mivutano ya kisiasa ndani ya serikali ya Somalia, ambayo imezuwia serikali kufanyakazi yake kwa ufanisi imesababisha ongezeko la hivi karibuni la uharamia. Uharamia katika taifa hilo la pembe ya Afrika umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni, na kufikia kukamatwa mwishoni mwa wiki kwa meli kubwa ya mafuta ya Saudi Arabia iliyochukua mafuta yasiyosafishwa yenye thamani ya dola milioni 100.
Jean Ping amelihusisha ongezeko hilo la uharamia na mpasuko ndani ya uongozi wa serikali ya mpito ya Somalia na kutoa wito kwa walinzi wa amani wa umoja wa mataifa kupelekwa katika taifa hilo haraka iwezekanavyo.
Rais huyo wa halmashauri kuu ya umoja wa Afrika ameeleza wasi wasi wake mkubwa kutokana na ongezeko la hivi karibuni la uharamia katika pwani ya Somalia, imesema taarifa ya umoja wa Afrika wiki hii.
Hii ni ishara wazi ya kuporomoka zaidi kwa hali ambayo italeta madhara makubwa zaidi kwa nchi hiyo, eneo lote la pembe ya Afrika pamoja na eneo kubwa la jumuiya ya kimataifa.
Ongezeko la uharamia limeingiliana na mapambano ya wapiganaji nchini Somalia, ambako wanamgambo wa Kiislamu ambao waliondolewa madarakani wamekuwa wakipigana kupata udhibiti tangu mapema mwaka 2007.
Serikali imekuwa ikijishughulisha zaidi na mapigano dhidi ya wapiganaji na kusahau juu ya uharamia, lakini pia katika miezi ya hivi karibuni imetumbukia katika mivutano ya ndani kisiasa.
Rais wa Somalia Abdullahi Yusuf Ahmed na waziri mkuu Nur Hassan Hussein wameshindwa kukubaliana kuhusu baraza jipya la mawaziri kwa miezi kadha. Wapiganaji wamechukua nafasi hii kwa kukamata miji kadha nchini Somalia na kuelekea karibu na mji mkuu Mogadishu.
Wakati huo huo maharamia , ambao wako kwa kiasi kikubwa katika jimbo lenye utawala wa ndani kaskazini ya Somalia la Puntland, wamezishambulia kwa makundi meli kadhaa, licha ya kuwapo meli za kivita za mataifa ya nje katika ghuba ya Aden.
Makampuni mengi ya meli sasa wanaepuka ama wanafikiria kuepuka kupitisha meli zao katika ghuba ya Aden, njia inayopitiwa na meli nyingi na ambayo ni sehemu ya njia inayounganisha bahari ya Hindi na ile ya Mediterranean kupitia mfereji wa Zuez.
Meli ya Sirius star ambayo ilitekwa nyara siku ya Jumamosi kiasi cha kilometa 830 kusini mashariki ya mji wa Mombasa nchini Kenya, imetia nanga karibu na bandari ya Somalia ya Harardhere, ikiwa ni moja kati ya vituo vya maharamia hao , wakati majadiliano juu ya madai ya malipo ya kuikomboa yakiendelea.
Wafanyakazi 25, kutoka Uingereza, Croatia, Philiippines, Poland na Saudi Arabia , kwa mujibu wa mmiliki wa meli hiyo wako salama na hakuna mipango ya ama majeshi ya kimataifa na maafisa wa jimbo la Puntland kuvamia meli hiyo.
Ongezeko la uharamia limesababisha ongezeko la doria inayofanywa na majeshi ya NATO, Urusi, majeshi yanayoongozwa na Marekani na Ufaransa katika pwani ya Somalia.
Umoja wa Ulaya pia umeidhinisha jeshi litakalokuwa na meli za kivita kati ya tano na saba, ambalo linatarajiwa kuwasili katika eneo hilo la ghuba ya Aden mapema mwezi Desemba. Kuwapo kwa jeshi kubwa la majini hakujawazuwia maharamia wakati wanadai fedha nyingi za kukomboa meli wanazoziteka, lakini wameanza hivi karibuni kupata hasara.
Jeshi la majini la India limesema wiki hii kuwa meli yake ya kivita ya INS Tabar ambayo imewekwa katika ghuba ya Aden ili kuchunguza nyendo dhidi ya maharamia pamoja na kufanya doria imeharibu meli moja ya maharamia.