Je, wajuwa? Hiki ndicho kipindupindu
17 Mei 2017Kipindupindu ni maradhi yanayoambukizwa kupitia kimelea kiitwacho kwa lugha ya kitaalamu vibrio cholerae, ambacho husambaa kupitia maji ya kunywa au chakula.
Kwa hivyo, kimsingi maradhi haya hupatikana kupitia uchafu kwenye maji na chakula na ni nadra sana kimelea hiki kusafiri kutoka mtu mmoja kwenda mwengine kupitia njia nyengine.
Vimelea vinapokuwa vingi sana, maambukizo yake yanaweza kuripuka ndani ya masaa machache tu, na huchukuwa takribani siku mbili hadi tatu.
Maambukizi haya huambatana na tumbo la kuharisha na wakati mwengine kutapika na hivyo mgonjwa kupoteza kiwango kikubwa cha maji mwilini. Mashambulizi ya vimelea yanapokuwa makubwa, mgonjwa anaweza kupoteza hata lita 20 kwa siku.
Asilimia 60 ya wagonjwa wanaokumbwa na maradhi haya hufariki dunia kama hawakupatiwa matibabu ya mapema na ya uhakika, kwa kuwa figo hushindwa kufanya kazi yake na mfumo wa usambazaji damu mwilini huporomoka moja kwa moja.
Asili ya maradhi haya ni kwenye Delta ya Ganges huko Asia ya Kusini, ambako yaligunduliwa kwenye karne ya 19, lakini kufikia karne ya 20 yakawa yameenea kote Asia, Afrika na Pasifiki.
Katika maeneo ambako usafi wa mazingira ni hafifu, hasa mataifa ya Asia na Afrika, kitisho cha kipindupindu kila mara huwa cha juu na msimu wa mvua kubwa mara nyingi huwa kichocheo cha kusambaa kwa uchafu huo na kuingia kwenye vyanzo vya maji yanayotumika majumbani.
Maji machafu yanapoongezeka na tatizo la upungufu wa lishe, ni rahisi sana maradhi ya kipindupindu kuangamiza maisha ya watu wengi kwa wakati mmoja.
Ingawa ugonjwa wa kipindupindu una kinga, lakini kinga hiyo huwa ya miezi michache tu na Shirika la Afya Duniani (WHO) halipendekezi matumizi ya chanjo kwenye kukabiliana na ugonjwa huu, bali limeweka msisitizo mkubwa zaidi kwenye usafi wa mazingira, maji salama na matibabu ya haraka pale yanapotokea.
Mwandishi: Mohammed Khelef/KNA
Mhariri: Saumu Yussuf