1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je viongozi wa G20 watafikia mwafaka?

Saumu Ramadhani Yusuf11 Novemba 2010

Viongozi wa G20 wajadiliana kuhusu mikakati ya kuzuia mporomoko mpya wa Kiuchumi

https://p.dw.com/p/Q5rh
Picha: Orgranisationskomitee G20 Seoul Summit

Viongozi wa kundi la G20 wanakutana huko Korea Kusini katika mkutano wao wa kilele utakaozungumzia masuala mbali mbali. Hata hivyo wakati viongozi hao wakikutana tayari imegusiwa kwamba mkutano huo unakabiliwa na kitisho cha kutofikiwa mwafaka juu ya kukiondoa  kizingiti kikubwa katika kuutatua mgogoro wa uchumi duniani.

Viongozi wa kundi la G20 wanakutana huku kukiweko hofu juu ya kuzuka kwa mporomoko mwingine wa kiuchumi ambapo tayari kuna ati ati kuhusu uwezekano wa nchi mojawapo ya kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Ireland kukumbwa na mzozo mpya ya kifedha.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamelazimika kuyapa matumaini masoko ya fedha muda mfupi baada ya kuwasili mjini Seoul kuhusiana na wasiwasi huo uliopo kwamba Dublin huenda ikahitaji msaada wa kuikwamua katika madeni yaliyopindukia viwango.

g20 Seoul angela merkel Barack Obama
Rais Barack Obama na Kansela Angela Merkel katika mkutano wa SeoulPicha: AP

Rais wa halmashauri ya Umoja huo wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema wanaifuatilia kwa karibu hali ya mambo huko Ireland na kwamba wamejiandaa kwa hali zote kuchukua hatua katika suala hilo. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pia amezungumzia wasiwasi uliopo kwa kusema

''Hakuna mtu anayetaka kuingia katika matatizo mengine ya kiuchumi, kwa hivyo sote tushirikiane kuukuza uchumi na kuuendeleza kama tulivyofanya mwaka mmoja uliopita''

Suala muhimu linalogubika mkutano huo ni kuhusu sera za mpango wa kusimamia viwango vya ubadilishanaji fedha suala ambalo limewaingiza katika mvutano viongozi wa nchi tajiri.

 Marekani na Umoja wa Ulaya wanaishutumu China kwa kuiweka sarafu yake katika viwango vya chini kwa lengo la kuzifanya bidhaa zake kuuzwa kwa bei nafuu, Wakati viongozi wengine wa dunia wakikasirishwa na hatua ya benki kuu ya Marekani ya kutumbukiza dolla millioni 600, katika uchumi wa taifa hilo unaokabiliwa na msukosuko, jambo ambalo limeifanya sarafu ya dola kuanguka thamani.

Hata hivyo rais Hu Jintao wa China amekanusha madai kwamba nchi yake inafanya kusudi kuiteremsha thamani sarafu yake ya Yuan kwa manufaa yake.

 Ama akizungumzia kuhusu haja ya kuishirikisha zaidi China katika kuutatua uchumi wa dunia, waziri mkuu wa Uingereza David Cameroon amesema.

''Watu hawawezi tena kuzungumzia uchumi wa dunia bila kuijumuisha China ambayo uchumi wake umeimarika kwa kiwango cha 10 asilimia kila mwaka katika miongo mitatu.''

NO FLASH Finanzministertreffen in Südkorea G20
Mwafaka uliofikiwa na mawaziri wa fedha wa G20 kuhusu IMF unajadiliwa Seoul

Wakati huo huo Katibu  Mkuu  wa Umoja  wa Mataifa  Ban Ki-Moon  amewataka viongozi wa nchi  tajiri  waitekeleze ahadi  ya kuuondoa umasikini duniani.Kauli ya Ban Ki Moon ni kwamba,

''Nitajitahidi niwezavyo kuhakikisha viongozi wa dunia wa nchi zenye uwezo mkubwa kiuchumi wanapata suluhisho katika mipango yao ya kuwasaidia watu maskini na wasiojiweza duniani''

Katika kikao cha leo na kesho viongozi hao wanatarajiwa pia kuidhinisha makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita na mawaziri wa fedha wa kundi hilo la G20 ya kulifanyia mageuzi shirika la fedha duniani IMF, mageuzi ambayo yatafungua njia kwa nchi zinazoinukia kiuchumi kama China na India kuwa na sauti kubwa ya kupitisha maamuzi katika chombo hicho.

Mwandishi Saumu Mwasimba/RTRE

Mhariri: Josephat Charo.