1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwekezaji wa Mashariki ya Kati watoa kitisho kwa Magharibi

14 Septemba 2023

Nchi za mashariki ya kati zimeimarisha vitega uchumi katika nchi za magharibi kuanzia klabu za kandanda hadi kampuni za simu. Je hilo ni tishio kwa nchi za magharibi?

https://p.dw.com/p/4WIO5
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: Saudi Press Agency/dpa/picture alliance

Nchi za kiarabu za ghuba zinaongeza kuwekeza katika nchi za magharibi kutokana na nguvu ya kupanda bei ya mafuta. Licha ya kuwanunua wanakandanda maarufu wa klabu za Ulaya Christian Ronaldo, Neymar na Benzema na kuwalipa  mamilioni ya Euro, Saudi Arabia wakati wote imefungua mifuko yake kuzipiga jeki biashara za nchi za magharibi.


Pamoja na majirani zake Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar, Saudi Arabia iliufungua mfuko wake mkubwa wa uwekezaji wakati wa mgogoro mzito wa kifedha mnamo mwaka 2008/2009 kuzisaidia benki kadhaa za nchi za magharibi licha ya uchumi wao kudhoofika kutokana na kuanguka bei ya mafuta. Mkurugenzi wa taasisi ya GIGA ya mitaala ya Mashariki ya Kati Eckart Woertz amesema mataifa ya Ghuba yanaweza  kuekeza kiwango kikubwa cha fedha bila ya urasimu hasa pale hali inapokuwa ngumu. Amesema nchi za ghuba aghalabu zimekuwa waokozi wa haraka.


Kwa sasa Saudi Arabia inazo hisa kwenye kampuni za Nintendo,Uber,Boeing na pia kwenye klabu ya kandanda, New Castle. Mnamo mwezi wa Juni chama cha golf PGA Tour kilifikia makubaliano ya utatanishi ya kuungana na chama  kingine cha golf LIV kinachofadhiliwa na Saudi Arabia. Makubaliano hayo yalishutumiwa na asasi za kutetea haki za binadamu. Kampuni nyingine ya Saudi Arabia PIF pia inamiliki karibu theluthi mbili ya wanaotarajia kuwa washindani wa Tesla, Lucid Motors, kwa  kumwaga dola bilioni 5.4 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye kampuni inayozalisha magari yasiyozidi 10,000 kwa mwaka.


Uwekezaji mkubwa pia unafanyika katika makampuni ya simu Ulaya

Nembo ya kampuni ya mawasiliano ya Saudi Arabia STC
Nembo ya kampuni ya mawasiliano ya Saudi Arabia STCPicha: Joan Cros/NurPhoto/picture alliance

Uwekezaji wa hivi karibuni, japo wa kiwango kidogo ulikuwa wa kampuni ya simu ya Saudi Arabia STC. Ilitangaza kuongeza asilimia 10 ya hisa katika kampuni ya simu ya Uhispania,Telefonica,yenye thamani ya dola bilioni 2.25. Katika kipindi cha miaka minane iliyopita, thamani ya soko ya kampuni ya Telefonica imepungua kwa theluthi mbili. Vita vya bei katika huduma za simu na mtandao, uwekezaji katika teknolojia mpya na upanuzi wa masoko mapya kwa pamoja  yamesababisha deni kubwa kwa kampuni hiyo ya Uhispania.


Kampuni ya simu ya UAE e& mwaka huu iliongeza hisa zake katika kampuni nyingine kubwa ya  Ulaya ya mawasiliano ya simu, Vodafone, kutoka asilimia 10 hadi karibu 15 asilimia. Mwezi uliopita, kampuni hiyo Umoja wa Falme za Kiarabu ilisema inatafakari kuongeza hisa zaidi, hadi asilimia 20.


Awamu hizo mbili za uekezaji zimezua wasiwasi juu ya usalama wa taifa, kutokana na mataifa ya Ghuba kuwa na tawala za kidikteta. Tawala hizo zina historia ndefu juu ya kukiuka haki za binadamu. Wiki iliyopita makamu wa waziri mkuu wa Uhispania Nadia Calvino alisema hisa zilizowekwa katika kampuni ya Telefonica zinapaswa kuchunguzwa kwa kuzingatia maslahi ya ulinzi ya  Uhispania.

Zipo taarifa kwamba Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zinanunua tekinolojia za mawasiliano kutoka Marekani. Nchi hizo zimesema wazi kwamba zinakusudia kuongoza katika teknolojia za akili bandia.Wahusika wa sekta hiyo katika nchi za magharibi wametahadharisha juu ya hatari ya teknolojia hizo kutumiwa na tawala za kidikteta.