1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je unaweza kubaini habari za uwongo?

3 Januari 2022

Kuna mfululizo wa taarifa za uwongo zinazosambaa mitandaoni kuhusu maudhui mbalimbali, kuanzia ugonjwa wa COVID-19, mabadiliko ya tabia nchi, uhamiaji na kadhalika.

https://p.dw.com/p/455lp
Fakt oder Fake Symbolbild
Picha: S. Ziese/blickwinkel/picture alliance

Taarifa za uwongo huenea haraka kwenye mitandao ya kijamii ukilinganisha na taarifa sahihi na za ukweli. Lakini unawezaje kutofautisha kati ya taarifa za kweli na za uwongo?

Taarifa za uwongo aghalabu huenea kwa kasi na limekuwa tatizo kubwa katika ulimwengu wa kidijitali.

Watumiaji wengi wa mitandao hupata ugumu kutenganisha taarifa za kuaminika na zile za kupotosha.

soma "Habari za uongo", kitisho cha uhuru wa vyombo vya habari

Kwa mfano mnamo Aprili mwaka uliopita 2021, picha ya nukuu iliyodaiwa kutoka kwa mwanasiasa wa Ujerumani Annalena Baerbock ilisambazwa kwenye Facebook. Ndani yake, kiongozi huyo wa Chama cha Kijani na aliyekuwa mgombea wa kiti cha Ukansela, anadaiwa kutoa wito wa kusitishwa kwa umiliki wa kibinafsi wa wanyama kwa sababu eti wanyama hutumia hewa nyingi sana.

Wakati wa janga la corona, video na machapisho ya wataalamu wa matibabu ambao taarifa zao kuhusu virusi hivyo zinakinzana na matokeo mengine ya kisayansi zilisambaa sana mitandaoni.

Je, kuna uhusiano gani kati ya mifano hii? Zote ni taarifa za uwongo, habari zenye kupotosha lengo likiwa ni, kwa makusudi kushawishi maoni ya kisiasa au kutafuta wafuasi wengi kwenye mitandao hiyo.

soma Kusambaa kwa habari za uwongo tishio kwa uandishi

Vipi unaweza kubaini habari ghushi?

Social Media Apps | WhatsApp Facebook Twitter Instagram
Picha: Nasir Kachroo/ZUMA Press/imago images

Kwanza kabisa kuwa muangalifu. Katika Ripoti ya hivi karibuni ya Habari za Dijitali kutoka Taasisi ya Reuters katika Chuo Kikuu cha Oxford, zaidi ya nusu ya waliohojiwa walisema hivi karibuni waliona habari za uwongo au za kupotosha kuhusu corona. Zaidi ya robo moja walikumbuka habari potofu katika muktadha huo kuhusu watu mashuhuri.

Mtu yeyote anayetumia mtandao wa intaneti anapaswa kuwa macho hasa kuhusu mada za hisia na utata au jambo linaloonekana kuwa la kuvutia sana na linaloonekana kuwa limetiwa chumvi.

Jaribu kufahamu ni wapi taarifa ilikotoka, nani aliyeisambaza?

Habari ghushi mara nyingi huwafikia watumiaji baada ya kuchapishwa kwenye majukwaa kama Facebook, Twitter au Instagram. Tazama kwa makini akaunti iliyotumiwa kueneza habari hiyo. Hilo linaweza kukusaidia kujua kuhusu lengo na madhumuni ya mchapishaji huyo.

3D Illustration | Fake News Lupe Facts
Picha: Alexander Limbach/Zoonar/picture alliance

Messenger ni mtandao mwengine ambao pia unatumika kusambaza habari za uwongo. Ukipokea ujumbe kupitia mtandao huu muulize aliyekutumia ni wapi alipoipata taarifa hiyo. Mara nyingi aliyekutumia, yeye pia huwa ametumiwa na bila ya kukagua uhalisia wake au chanzo anaisambaza pia.

Ikiwa ujumbe umeambatanisha kiungo tovuti, unaweza pia kuangalia ni kituo gani au kurasa zingine walizochapisha. Kiungo tovuti ndani ya ujumbe haimaanishi kuwa habari hiyo ni sahihi. Kuna tovuti ambazo sio za kuaminika na zinategemea propaganda na kutia chumvi kwa ajili ya kujiongezea ufuatiliaji.

soma Makala Maalum : Mfumo mpya wa tovuti.

Pia nikupe onyo, kuna baadhi ya viungo tovuti ukibonyeza kusoma au kutazama video, zinatumia bando yako kwa njia za kijanja, ukiambiwa uweke namba zako za siri au taarifa zako binafsi katika maeneo ambayo sio stahiki, hizo ndio tovuti ghushi.

Njia nyengine ya kubaini iwapo taarifa au video ni ya kweli, jiulize je madai haya ni ya kweli?

Ni muhimu kuchunguza kwa undani maudhui halisi ya chapisho, ujumbe uliotumwa au maandishi mengine yoyote. Je, madai au picha hizo zinashikamana na ni za kweli?

Pia usisambaze kila chapisho unalotumiwa, Kama mtumiaji wa mtandao, unaweza kuchukua hatua ili kukabiliana na ushawishi mbaya wa habari ghushi kwa kutosambaza kile ambacho umetumiwa bila uangalifu. Taarifa za uwongo hazisambazwi kwa nia mbaya au imani fulani, bali kwa sababu ya kutozingatiwa au kwa sababu ya kuchochewa na hisia kali.