Je Ulaya itaweza kushinikiza dunia juu ya mageuzi ya fedha ?
6 Novemba 2008Viongozi wa Ulaya tayari wamesema kwamba wanataka mataifa makubwa duniani kuanzisha aina mpya ya ubepari.
Waziri wa Fedha wa Sweden Anders Borg ameulezea mjadala huo kwa lugha hii kwamba kwanza na pengine jambo muhimu kabisa ni kwamba wanahitaji sana kuwa na idara ya zima moto inayofanya kazi kikamilifu kwamba hatimae waweze kuwa na majadiliano ya kanuni za usalama wa moto kwa ajili ya majengo.Hadi sasa nchi tatu wanachama wa Umoja wa Ulaya yaani Uingereza,Ufaransa na Uholanzi zimesambaza nyaraka miongoni mwa nchi wanachama wenzao wa umoja huo zikielezea jinsi zinavyofikiria msimamo wa Umoja wa Ulaya unavyopaswa kuwa katika mazungumzo ya Washington ya tarehe 15 mwezi wa Novemba.
Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya hapo Jumanne walipunguza makali ya rasimu ya awali ya waraka wa mapendekezo ya Ufaransa kutokana na kuwa na maelezo mengi mno na kuashiria kwamba bado kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Hali hiyo imewafanya viongozi wa Umoja wa Ulaya mazungumzo yao kuwa ya kukata na shoka wakati wakijaribu kuwa na msimamo wa pamoja wa Umoja wa Ulaya.
Nyaraka za nchi hizo tatu ambazo shirika la habari la Ujerumani la Deutsche Presse imeziona zinafanana katika vipengele vikuu lakini zinatafautiana juu ya namna ya kutekelezwa kwa vipengele hivyo.
Kwa mfano nyaraka zote tatu zinatowa wito wa kutanuliwa na kuimarishwa kwa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na Baraza la Uthabiti wa Fedha FSF la benki kuu kubwa duniani na wizara za fedha.
Nyaraka hizo pia zimeipa umuhimu haja ya kufanyia mageuzi taasisi za mikopo na kanuni za vyombo vya mahesabu na kuboreshwa kwa suala la marupurupu na uwazi ndani ya sekta za fedha.
Hata hivyo wakati zinakubaliana juu ya vipengele muhimu nyaraka hizo zinatafautiana juu ya suala la kwa kiasi gani taasisi za kimataifa ziruhusiwe kuratibu masoko ya kitaifa.
Wakati nyaraka za Uholanzi na Ufaransa pia zikitaka Baraza la Uthabiti wa Fedha FSF liwekwe rasmi chini ya kivuli cha Shirika la Fedha la Kimtaifa IMF Uholanzi inataka IMF kuwa shirika kuu litakalowajibika na utahibiti wa fedha duniani kusimamia mashirika yote mengine na kuwa na mamlaka ya kutowa mapendekezo kwa serikali za taifa.
Wito huo yumkini ukakabiliwa na upinzani kutoka nchi ambazo zinataka kulinda taasisi zao za kitaifa.
Na hatimae nyaraka za nchi hizo tatu zinatafautiana juu ya suala kwa undani gani kampuni za fedha zinapaswa kuratibiwa katika kipindi cha usoni.
Duru kutoka Brussels zinasema kwamba viongozi hao wa nchi za Umoja wa Ulaya wako hatarini kuzusha mzozo juu ya suala la nani anayepaswa kuhudhuria mkutano wa viongozi wa nchi wa Washington huku Uhispania ikisisitiza kwamba inapaswa kuwepo mjini Washington kutokana na kuwa mojawapo ya mataifa makubwa ya kiuchumi ya Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Luxembourg mwenye ushawishi Jean-Claude Juncker pia inasemekana kuwa amevunjika moyo kwa kutoalikwa kwa kuzingatia cheo chake cha kuwa mkuu wa kundi la nchi zenye kutumia sarafu ya euro barani Ulaya.