Je Ukraine itaenedelea kupokea gesi kutoka Urusi?
18 Mei 2018Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Urusi Vladimir Putin kwenye mazungumzo yao wamejadiliana kuhusu mgogoro wa nchini Ukraine, wakati ambapo Urusi inaongeza ukubwa wa bomba lake la gesi ya asili kwenda moja kwa moja hadi nchini Ujerumani, bila kupitia Ukraine.
Rais Putin na Waziri wake Mkuu Dmitry Medvedev walimkaribisha Kansela Merkel katika makao ya rais ya majira ya kiangazi yaliyopo katika jiji la kusini mwa Urusi la Sochi, kansela Merkel ndiye aliyeongoza vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi wakati nchi hiyo ilipolitwaa jimbo la Crimea miaka minne iliyopita.
Lakini katika miezi ya hivi karibuni, Ujerumani ilitoa idhini yake kwa Urusi kuweza kutanua bomba lake la gesi la Nord Stream, ambalo litasafirisha gesi ya asili hadi nchini Ujerumani licha ya Ukraine kuupinga mradi huo na kusema kwamba unakiuka vikwazo dhidi ya Urusi. Waziri wa uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier, ameitembelea Ukraine mara mbili wiki hii ili kuihakikishia nchi hiyo msaada wa Ujerumani.
Mkutano wa viongozi hao unatarajiwa kutoa nafasi mpya ya kujadili mambo mengine na pia Ujerumani na Urusi zote zinataka kuokoa mpango wa nyuklia wa Iran baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi yake kutoka kwenye mpango huo.
Uhusiano wa Ujerumani na Urusi unakabiliwa na vizingiti kadhaa. Kwanza ni kuhusu Mashambulizi ya mtandaoni ambapo Idara ya ujasusi ya nchini Ujerumani inaamini kwamba Urusi inahusika na mashambulizi katika mitandao ya Ujerumani. Kwa mfano mashambulizi dhidi ya mtandao wa Bunge la Ujerumani ya mwaka 2015, pamoja na kwenye mitandao binafsi ya vyama vya kisiasa na pia kwenye wakfu za hapa Ujerumani.
Pia idara ya usalama wa ndani ya nchini Ujerumani, BfV, inaishutumu Urusi kwa kuhusika na shambulio katika mtandao wa serikali ya Ujerumani la mwezi Februari mwaka huu wa 2018 ambapo kiwango kikubwa cha data kiliibiwa.
Mengine ni kuhusu jukumu la Urusi huko nchini Syria, Urusi kulitwaa jimbo la Crimea, tabia ya ushari, maendeleo duni huko mashariki mwa Ukraine, vikwazo vya usafiri na unyanyasaji. Kansela Merkel amesema Urusi lazima ihusishwe katika mchakato wa kutafuta amani nchini Syria.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPA / p.dw.com/p/2xsjx
Mhariri: Grace Patricia Kabogo