Ushauri wa kuchukuliwa tahadhari.
26 Juni 2020Jee milipuko iliyozuka nchini Ujerumani pia itafika mbali? mwezi Machi kitongoji cha mapumziko cha Ischgl katika nchi jirani ya Austria kilikuwa kitovu cha kueneza maambukizi kwa kiwango kikubwa ndani ya nchi hiyo na mbali kwa majirani. Wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza pamoja na viongozi hawaoni uwezekano wa kutokea hatari hiyo hata hivyo wanasema pana haja ya kuchukua tahadhari. Mjadala umezuka baada ya kulipuka maambukizi kwenye wilaya mbili za jimbo la NorthRhine Westphalia magharibi mwa Ujerumani.
Katika kitongoji cha burudani cha Ischgl nchini Austria ambapo pana shughuli nyingi za kitalii maambukizi yalizuka na kuenea haraka barani Ulaya. Waendesha mashtaka wa serikali nchini humo sasa wanaangalia uwezekano wa kuanzisha uchunguzi dhidi ya viongozi wa mji huo ili kubainisha iwapo walisababisha hatari ya magonjwa ya kuambukiza. Ziko picha zinaonyesha jinsi watu wa mji huo walivyokuwa wanaburudika kwenye tafrija huku wakikaribiana wakati maambukizi yalikuwa yanaenea duniani kote.
Karantini yawekwa tena
Kuhusu nchini Ujerumani kwa mara ya kwanza hatua zilizowekwa kwa ajili ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi zililegezwa hivi karibuni baada ya wimbi la kwanza. Hata hivyo hatua hizo zimerudishwa tena kwenye wilaya mbili. Uamuzi huo umechukuliwa baada ya kulipuka maambukizi kwenye kiwanda cha kusindikia nyama kinachomilikiwa na kampuni inayoitwa Tönnies katika wilaya ya Gütersloh iliyoko kwenye jimbo la NorthRhine Westphalia magharibi mwa Ujerumani.
Soma zaidi:Serikali Ujerumani zatofautiana kuhusu kuondoa vizuizi
Maambukizi pia yalilipuka kwenye wilaya jirani ya Warendorf.Hatua za karantini zimewekwa tena kwenye wilaya hizo mbili sawa na zile zilizowekwa mnamo mwezi machi. Shule na kindagateni zimefungwa tena.
Wataalamu wana matumaini
Hatua zilizochuliwa kwenye wilaya hizo mbili ni za tahadhari. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kwenye taasisi ya utafiti ya Bremen, Hajo Zeeb amesema anatumai maambukizi yaliyotokea katika sehemu hizo mbili yatapungua. Mtaalamu huyo amesema mlipuko wa maambukizi kwenye kiwanda cha nyama hapa nchini Ujerumani yamewakumba wafanyakazi kutoka nchi za Ulaya Mashariki wanaokuja Ujerumani kwa misimu. Kiwanda hicho sasa kimefungwa. Wenyeji wengi wa sehemu za karibu na kiwanda hicho wamepimwa na matokeo yameonyesha kuwa ni watu wachache waliaombukizwa kulinganisha na sehemu nyingine.
Wafanyakazi kutoka Ulaya Mashariki
Watu 1500 kwenye kiwanda hicho cha nyama wameambukizwa. Wanasiasa na wafanyabiashara wamelaumiwa juu ya mambukizi hayo kwa sababu walijua siku nyingi juu ya hali mbaya kwenye kiwanda hicho. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza Zeeb ameeleza kwamba hatua zingeliweza kuchukuliwa mapema.
Msemaji wa chama cha kijani Helge Braun pia amekemea mazingira mabovu ya kazi kwenye kiwanda hicho cha nyama. Wafanyakazi wanaotoka nchi za Ulaya Mashariki wanawekwa katika mazingira hayo mabovu. Msemaji huyo ameonya kwamba ikiwa hatua za tahadhari hazichukuliwi maambukizi yatalipuka tena nchini lakini Ujerumani imeweza kuepuka hali kama ile ya mji wa Ischgl wa nchi jirani ya Austria angalau kwa sasa!
Chanzo: DW