Je, Rais Bola Tinubu ndio suluhu ya matatizo ya Nigeria?
28 Juni 2023Miongoni mwa changamoto hizo nyingi zinazoikabili Nigeria ni mzigo mkubwa wa madeni, kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, na uhaba wa nishati muhimu ya umeme ambayo kwa miaka mingi imekuwa kikwazo katika ukuaji wa kiuchumi.
Lipo pia tatizo la kupungua kwa uzalishaji wa mafuta ghafi, na ukosefu wa usalama umbao umeiacha serikali kuu ikikosa uwezo wa kuyadhibiti maeneo mengi ya nchi.
Jason Tuvey, mkurugenzi anayehusika na masoko yanayoinukia katika kituo cha Capital Economics, anasema ingawa yamefanyika mageuzi makubwa ya kisera, bado yapo mambo ambayo wawekezaji wangependa kuyaona yakifanyika.
Soma pia: Nigeria wapambana kununua mafuta kabla ya ruzuku kuondolewa
Wachambuzi wanasema itakuwa kazi ngumu kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo, kwa hoja kwamba ufisadi uliokita mizizi na mitandao ya upendeleo vinaendelea kushuhudiwa nchini Nigeria.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni moja ya kifedha mjini Lagos Bismarck Rewane, anasema ni kazi ngumu sana kuzitenganisha siasa za Nigeria na ufisadi.
''Njia ya kufika katika madaraka kisiasa nchini Nigeria mara zote hupitia katika uchochoro wa kimaslahi. Ukitaka kuwafungia njia mafisadi watapambana na wewe. Inahitaji ujasiri na dhamira ya dhati kuwaambia, ''angalia, tunayafanya haya ili kulinusuru taifa'', na kwamba ili kufanikiwa unahitajika mfumo wenye usawa.''
Rais Tinubu afuta riziki ya mafuta ya Petroli
Siku chache tu baada ya kuchukua hatamu za uongozi, Rais Bola Tinubu alifuta ruzuku kwa mafuta ya petrol iliyodumu kwa miongo kadhaa, alimsimamisha kazi gavana wa benki kuu, na kuachia hazina ya fedha za kigeni.
Itachukua muda mrefu kwa matunda ya juhudi hizi za mageuzi kudhihirika, na kuendelea kuyasimamia mageuzi hayo haitakuwa rahisi.
Kupitia hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni, Tinubu alihimiza kuachana na ruzuku ya mafuta, kwa maelezo kwamba fedha zitakazokusanywa zitatumiwa kuboresha elimu, mfumo wa afya na kuimarisha ugavi wa nishati ya umeme.
Kufuatia kuondolewa kwa ruzuku hiyo, bei ya bidhaa hiyo imeongezeka mara tatu, na kuathiri vibaya mamilioni ya familia na biashara ndogo ndogo ambazo zilitegemea nishati hiyo kwa sababu gridi ya umeme nchini Nigeria inasuasua.
Nauli pia imepanda kwa wafanyakazi wanaosafiri kwenda kazini na wakulima wanaopeleka mazao yao sokoni. Dereva mmoja wa teksi mjini Lagos, Tunau Taiwo analalamika akisema Tinubu alijinadi kama mtu bora kabisa kwa kazi ya urais, lakini sasa sasa ameanza kuwatesa raia. Je hali itakuwaje baada ya miezi sita? anajiuliza dereva huyo.
Wakati huo huo, ushindi wake wake bado unalalamikiwa mahakamani. Nnamdi Obasi, mshauri mkuu wa shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG nchini Nigeria, anasema Tinubu ameirithi nchi iliyo na machungu, na anapaswa kuleta mageuzi yanayokubaliwa na umma, ikizingatiwa kuwa uhalali wa mamlaka yake bado una kasoro.
Soma pia:Wanigeria waandamana kupinga matokeo ya uchaguzi
Ukosefu wa usalama ni kizungumkuti kingine katika mipango ya rais Bola Tinubu. Wakati mtangulizi wake, Muhammadu Buhari alipoingia madarakani mwaka 2015, wengi walitumai kuwa jenerali huyo msaafu angefanikiwa kuyadhibiti makundi yenye silaha.
Ghasia zaibuka upande wa kaskazini mwa Nigeria
Matokeo yalikuwa kinyume, kwani ghasia ambazo kabla ya hapo zilikuwa tu upande wa kaskazini zilienea na kusambaa katika sehemu nyingine za nchi.
Wiki iliyopita Tinubu alifanya safisha safisha, akawafuta kazi mkuu wa usalama na kamishna mkuu wa polisi.
Hatua hiyo lakini haimuondolei vikwazo vyote, kwani jeshi la Nigeria lina mitandao yake ya uteja na kulindana. Kwa mfano, wachambuzi wanasema makundi yenye silaha katika mkoa wa delta yanatorosha mamilioni ya mapipa ya mafuta, wakisaidiwa na baadhi ya wanasiasa.
Soma pia:Maoni: Uchaguzi wa Nigeria na mwanga wa matumaini
Hata magenge yanayowachukuwa watu mateka kaskazini magharibi mwa Nigeria inasemekana yanaungwa mkono na serikali za majimbo.
Kipimo cha mafanikio ya Tinubu kitakuwa namna atakavyofanikiwa kuivunja mitandao hiyo ya rushwa na uhalifu, lakini wachambuzi wanasema hawana matumaini makubwa kuwa anao utashi wa kutosha wa kufanya hivyo.