China: Sera ya kuzuia kuenea Uviko-19 ni ya kulaumiwa?
13 Desemba 2022Jumba ambapo moto uliwaka ni mahala pazuri pa kuishi. Wafanyabiashara tajiri na familia zao walikuwa wanaishi hapo kwenye mji wa Urumqi uliopo katika jimbo la Xinjiang. Lakini maafa ya moto yalitukia. Janga hilo lilitokea mwezi uliopita katika ghorofa ya 15. Kwa mujibu wa taarifa ya maafisa wa serikali watu 10 walikufa na wengine 9 walijeruhiwa. Hata hivyo baadhi ya watu wamekanusha taarifa hiyo na wamesema kuwa watu wengi zaidi walikufa. Kutokana na sera ya China ya kubana vyombo vya habari na internet ni vigumu kupata taarifa za kuaminika na hasa kwenye mji wa Xinjiang.
Ni jambo la uhakika kwamba wazima moto walitatizika katika kufika mahala pa ajali. Wazima moto walionekana wakiuzima moto kwa mipira mirefu ya maji. Hata hivyo maji hayakufika kwenye sehemu zilizohitajika. Wazima moto pia walionekana wakijaribu kuondosha vizingiti vilivyowekwa kwa ajili ya kuyadhibiti magari barabarani. Muda haukutosha kutokana na msongamano wa magari uliosababishwa na sera kali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Mkurugenzi wa huduma za usalama amesema gesi hatari zilizosababisha vifo vya haraka zilikuwamo ndani ya nyumba. Wakati moto ulipozuka, mji wa Urumqi ulikuwa umewekwa katika karantini na kwa ajili hiyo ulifungwa kabisa kwa siku zaidi ya 100.
Mitandao ya kijamii nchini China ilijaa pomoni maelezo juu ya mshangao na uchungu watu walisema yumkini hatua kali za kuzuia maambukizi ndizo zilizosababisha vifo vya watu. Lakini jee ndivyo ilivyokuwa? walioshuhudia waliiambia DW kwamba watu hawakuweza kukimbia haraka kwa sababu waliokuwamo ndani ya nyumba walizuiwa ndani ya makaazi yao. Picha za mitandaoni zilionyesha milango iliyofungwa kwa kufuli ili kuwazuia kutoka nje wale waliokuwa wameambukizwa. Hatua za kuzuia maambukizi zilichangia katika kuzuka kwa janga hilo la moto lakini maafisa wa serikali wamewalaumu wananchi.
Baadhi ya watu hawakuwa na uwezo wa kujinusurisha kutokana na kuishiwa nguvu. Miongoni mwa waliokufa ni mama mmoja na watoto wake wanne. Mdogo kabisa alikuwa na umri wa miaka mitano. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya watu walioshuhudia, wamesema njia za usalama kwenye jengo zilikuwa zimefungwa. Ndiyo kusema watu walilazimika kutumia ngazi ili kujinusurisha. Haifahamiki ni kwa kiwango gani waokozi waliweza kuwaokoa watu haraka. Masaa kadhaa yalihitajika ili kuweza kuuzima moto.
Hakuna anayethubutu kusema ukweli. Waliojaribu kufanya hivyo kwenye mitandao ya kijamii wameadhibiwa kwa kupigwa faini au kwa kutiwa ndani. Polisi ya mji wa Urumqi kwenye jimbo la Xinjiang wamesema walimkamata mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 24 kwa kilichodaiwa kuwa alitoa habari za kupotosha. Kwa watu wanaotoka jimbo hilo ambao sasa wanaishi nje ya nchi, janga la moto lilitoa fursa ya kuwasiliana na ndugu zao lakini fursa hiyo haikuchukua muda mrefu.
Wakati huo huo China imeashiria utayari wa kulegeza hatua kali ilizochukua ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Taratibu hizo zimelegezwa kwenye wilaya na miji kadhaa iliyokumbwa na ongezeko la maambukizi. Makamu wa waziri mkuu wa China amesema nchi hiyo inakabiliwa na hali mpya.