Je, Afrika iko tayari kuushinda ugaidi?
5 Septemba 2014Tarehe 21 Septemba 2013 wanamgambo wa al-Shabaab walilivamia jengo la maduka la Westgate jijini Nairobi, Kenya, ambako waliwauwa watu zaidi ya 60, huku ikivichukuwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo siku nne kuukomeshwa mzingiro wa jengo hilo. Mwaka mmoja baadaye, taarifa za uhakika juu ya namna tukio hilo lilivyotokea - kama vile idadi ya washiriki na njia zilizotumika - bado hazijapatikana.
Kisha baina ya tarehe 14 na 17 Juni 2014, wanamgambo wakavamia kijiji cha Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, na tena wakawauwa watu zaidi ya 60. Bila ya shaka, orodha ya mauaji mengine yenye sura kama hiyo imekuwa ikiendelea.
Aprili 2014, kundi la Boko Haram liliwateka nyara wasichana 276 kutoka kijiji cha Chibok, jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Hadi sasa, Boko Haram imeshateka watu wengine kadhaa na huku wengi wa waliowateka awali wakiwa bado mikononi mwao.
Mwanzoni mwa Septemba 2014, viongozi wa Afrika walikutana jijini Nairobi, Kenya, kuujadili ugaidi, ambapo mwenyeji wao, Rais Uhuru Kenyatta, aliwaambia wenzake ugaidi Afrika ni uhalisia sasa.
"Ni jambo la kutia wasiwasi barani Afrika hivi leo kuona namna makundi ya kigaidi yalivyoongezeka kwa idadi na kwa uwezo. Boko Haram inaendelea kuzitia mashakani sehemu za mataifa ya Nigeria, Chad na Cameroon kwa mbinu mpya, kama vile kuwateka nyara wasichana 200 hivi karibuni, pia tuna al-Qaida tawi la Maghreb." Alisema Kenyatta kwenye mkutano huo.
Ugaidi ndio mada yetu leo Mbele ya Meza ya Duara, tukiangalia uzito wa kitisho hiki, athari zake na, kubwa kuliko yote, uhalisia wake na uwezo wa bara la Afrika kukabiliana nao. Kaskazini, eneo liitwalo Sahel, kuna tawi la al-Qaida la Maghreb, magharibi kuna Boko Haram, mashariki kuna al-Shabaab, na kama alivyosema Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kwenye mkutano huo wa Nairobi, kitisho hiki kinavuuka makundi moja moja tu, na kuwa muunganiko wa makundi mengine kadhaa ya kihalifu na kigaidi kwa pamoja.
"Kitisho hiki kinakuwa changamano zaidi kwa kukuwa kwa mafungamano kati ya ugaidi na uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, hasa hasa madawa ya kulevya na magendo ya silaha, biashara haramu ya binaadamu, na utakatishaji fedha zinazopatikana kwa njia haramu."
Kwa mujibu wa Rais Idriss Deby wa Chad, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika, mkutano huo wa Nairobi ulizungumzia uwezekano wa kuwa na mfuko wa pamoja kupambana na ugaidi barani Afrika.
Lakini je, hilo kweli linawezekana? Je, Afrika inaweza kupambana na ugaidi kwa nguvu na uwezo wake wote, kiwango ambacho inakabiliana na mengine? Je, mkutano huu wa Nairobi ulikuja wakati tayari umeshachelewa? Juu ya yote, sababu za ugaidi barani Afrika ni zipi?
Kuchambua mada hii, Mohammed Khelef anaongoza majadiliano kati ya Maggid Mjengwa, ambaye ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa za Afrika na mwanaharakati akiwa Iringa, Tanzania; Ally Saleh, ambaye ni mwanasheria, mwandishi wa habari wa kimataifa na pia mwanaharakati wa haki za binaadamu, Zanzibar, na Werunga Simiyu, mchambuzi wa masuala ya usalama kutoka Nakuru, Kenya.
Kusikiliza majadiliano yote, tafadhali bonyeza alama ya spika za masikioni hap