Jaribio la kombora la Korea Kaskazini lashindwa
22 Machi 2017Jaribio hilo la kombora limefanyika kutoka katika mji wa karibu wa Wonsan ulioko upande wa pwani mashariki mwa Korea Kaskazini ikiwa ni sehemu ile ile ambayo nchi hiyo mwaka jana ilifyatua makombora kadhaa ya masafa ya kati ambapo moja kati ya makombora hayo lilishindwa.
Msemaji wa vikosi vya Marekani katika ukanda wa Pasifiki Dave Benham amethibitisha kushindwa kwa kombora hilo mara tu baada ya kufyatuliwa na kuongeza kuwa kombora hilo limeripuka sekunde chache baada ya kurushwa. Haikuweza kufahamika mara moja ni kombora la aina gani lililorushwa na Korea Kusini ilikuwa ikifuatilia suala hilo kwa ajili ya kutoa taarifa zaidi.
Kuongezeka kwa idadi ya majaribio ya makombora kumeibua hali ya tahadhari kuhusiana na jinsi gani ulimwengu unaweza kukabiliana na hatua hiyo ya Korea Kaskazini.
Korea kaskazini ilirusha makombora manne ya masafa marefu kutoka eneo la jirani na upande wa pwani magharibi mwa nchi hiyo mnamo Machi 6, na pia wiki hii ilifanya jaribio la kombora la kinyuklia huku kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un akisema hatua hiyo imefungua ukurasa mpya katika mchakato wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Hatua hii inakuja baada ya mjumbe maalumu wa Marekani kuhusiana na sera za Korea Kaskazini, Joseph Yun kukutana na mwenzake wa Korea Kusini mjini Seul kujadili jinsi ya kukabiliana dhidi ya hatua zinazohusiana na mpango wa silaha kali wa Korea Kaskazini.
Marekani yajadili jinsi ya kukabiliana na uchokozi wa Korea Kaskazini
Wiki iliyopita Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alizuru Japan, Korea Kusini na China na suala linalohusiana na jinsi gani wanaweza kukabiliana na hatua hiyo ya Korea Kaskazini lilikuwa ni suala kubwa katika mazungumzo yake.
Tilerson alisema sera inayohusiana na uvumilivu juu hatua hizo za majaribio ya makombora zinazofanywa na Korea Kaskazini sasa umefikia mwisho, na kuwa mjadala juu ya kuchukua hatua nyingine dhidi ya taifa hilo ikiwa ni pamoja na hatua za kijeshi hivi sasa uko mezani iwapo Korea Kaskazini itafanya vitendo vya uchukozi dhidi ya Marekani au Korea Kusini.
Korea Kaskazini imefanya majaribio mawili ya makombora ya nyukilia pamoja na majaribio ya makombora kadhaa tangu mwanzoni mwa mwaka jana ikikaidi azimio la Umoja wa Mataifa na inaaminika kuwa iko katika mchakato wa kutengeneza silaha za nyukilia ambazo zinaweza kuizuru Marekani.
Mwandishi: Isaac Gamba/ rtre
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman