Jaribio la Korea Kaskazini lautia ulimwengu wasiwasi
4 Septemba 2017Kupitia mazungumzo ya simu, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amekubaliana na mwenzake wa Japan Taro Kono kuiwekea mbinyo zaidi Korea Kaskazini na kuwa wanataka mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili uwezekano wa kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vipya. Mattis ameionya vikali Korea Kaskazini kuwa itajibiwa kwa nguvu zote walizo nazo.
Rais wa Marekani Donald Trump alifahamishwa kuhusu kila njia ya kijeshi inayoweza kutumika dhidi ya Korea Kaskazini katika mkutano na timu yake ya usalama wa taifa. Trump amelaani vikali jaribio hilo na kusema kwamba ni kitendo cha uadui na kitisho kikubwa kwa Marekani.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, mazungumzo ya simu kati ya Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais wa Korea Kusini Moon Jae yaliafikia kuunga mkono azimio jipya dhidi ya nchi hiyo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Korea yalaaniwa na Jumuiya ya Kimataifa
Viongozi wengine ulimwenguni pia wameshutumu vikali jaribio hilo la Korea Kaskazini. China, Japan na Urusi zimelaani vikali. Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ametaka kutekelezwa haraka kwa vikwazo ambavyo tayari vipo na kuzingatia kwa dharura hatua mpya dhidi ya Korea Kaskazini.
Uingereza imesema China inahitaji kuiongezea Korea Kaskazini shinikizo la kiuchumi. Umoja wa Ulaya umesema unazingatia kuiwekea nchi hiyo vikwazo vikali zaidi.
Baraza hilo linafanya mkutano wake wa pili wa dharura kuhusu Korea Kaskazini katika kipindi cha juma moja baada ya jaribio hilo la jana la bomu la Haidrojen linalotajwa kuwa na nguvu iliyozidi bomu la kinyuklia lliloangushwa mji wa Hiroshima nchini Japan wakati wa vita vya pili vya dunia.
Je Korea Kaskazini itabinywa zaidi?
Mkutano huo ni kufuatia ombi la Marekani, Japan, Ufaransa, Uingereza na Korea Kusini. Mkutano huo wa leo unatarajiwa kuilaani zaidi nchi hiyo na kujadili hatua nyingine kali dhidi yake.
Huku hayo yakijiri wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imesema leo imegundua ishara kuwa Korea Kaskazini inatayarisha jaribio jingine la kombora na kuongeza huenda likawa kombora la masafa marefu. Hata hivyo haijaeleza bayana kuhusu ripoti hizo za jaribio jingine au ni lini litafanyika.
Maafisa wa wizara hiyo ya ulinzi wameliambia bunge la Korea Kusini kuwa bomu la jana Jumapili lilikuwa na nguvu ya kiloton 50. Marekani na Korea Kusini zimetangaza zitatuma mifumo zaidi ya kuzuia mashambulizi ya makombora.
Mfumo wa kuzuia makombora ujulikanao THAAD tayari umeshawekwa Korea Kusini, hatua ambayo imeikasirisha China lakini taarifa kutoka wizara ya ulinzi imesema mifumo mingine minne kama huo itatumwa hivi karibuni ili kujihami dhidi ya mashambulizi ya kinyuklia na ya makombora kutoka Korea Kaskazini.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa
Mhariri:Iddi Ssessanga