Japan yazindua mkakati mpya wa ulinzi
16 Desemba 2022Japan leo imezindua mkakati mpya wa ulinzi wa taifa utakaoiwezesha kutanua uwezo wake wa kijeshi kwa kumiliki makombora ya masafa marefu na mifumo mamboleo inayotumika kwenye vita vya mtandao.
Tangazo hilo linaakisi mabadiliko makubwa ya kisera ndani ya taifa hilo la Asia ambalo tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia limejizuia kuimarisha sekta yake ya ulinzi ikiwa ni pamoja na marufuku ya kumiliki silaha nzito.
Chini ya mpango huo mpya wa kiasi dola bilioni 300, Japan inalenga kujenga uwezo wa kujibu uchokozi kwa kununua meli za kisasa za kivita, makombora 500 ya masafa marefu na mifumo ya ulinzi ya ardhini.
Inaaminika mageuzi hayo yamechochewa kwa sehemu kubwa na kuongezeka kwa mivutano na mataifa jirani ya China, Urusi na Korea Kaskazini ambayo yanawekeza katika mifumo ya kisasa ya ulinzi na vita.