1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Japan yakumbuka miaka 75 ya bomu la atomiki Hiroshima

6 Agosti 2020

Japan imefanya kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuangushwa kwa bomu la kwanza la atomiki kwenye mji wa Hiroshima, huku meya wa mji huo akiitaka jumuiya ya kimataifa kuukataa ule aliouita uzalendo uliojengwa kwenye ubinafsi.

https://p.dw.com/p/3gUcq
Japan I Zeremonie zum Jahrestag in Hiroshima
Picha: Reuters/Kyodo

Hakukuwa na mkusanyiko wa maelfu ya watu kwenye Bustani ya Amani katikati ya mji wa Hiroshima kama inavyokuwa kwenye miaka mingine. Janga la virusi vya korona vilivyosambaa kote duniani limezifanya kumbukumbu za mwaka huu kukosa mahudhurio yake ya kawaida.

Watu pekee walioruhusiwa kuhudhuria kumbukumbu hizo ni manusura wa mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani pamoja na familia zao. 

Majira ya saa mbili na robo asubuhi ya tarehe 6 Agosti 1945, ndege ya kijeshi ya Marekani chapa B-29 Enola Gay iliangusha bomu lililopewa jina la "Mvulana Mdogo" na kuwauwa hapo hapo watu 140,000 kati ya wakaazi 350,000 wa mji huo.

Maelfu ya wengine walikufa siku za baadaye kutokana na majeraha na mionzi ya atomiki. Alkhamis ya leo, katika muda huo huo bomu hilo liliporipuka, watu walisimama na kunyamaza kimya kwa muda kuwakumbuka wahanga hao. 

Meya Kazumi Matsui wa Hiroshima alisema kwamba ni kuzuka kwa hisia kali za utaifa ndiko kulikopelekea Vita vya Pili vya Dunia na mabomu ya atomiki, jambo ambalo halipaswi tena kuachwa likarejea.

"Jamii iliyostaarabika inapaswa kuukataa uzalendo uliojikita kwenye ubinafsi na uungane dhidi ya vitisho vyote," alisema meya huyo.

Dunia bila nyuklia?

Hiroshima I Ausstellung Los Alamos
Picha hii ya tarehe 7 Septemba 1945 ilipigwa mahala ambapo mwezi mmoja nyuma yake bomu la atomiki liliangamiza maisha ya watu zaidi ya 140,000 mjini Hiroshima, Japan.Picha: picture-alliance/AP Photo/File/S. Troutman

Kuangushwa bomu kwenye mji huo wa Hiroshima kulifuatiwa na bomu jengine lililoangushwa Nagasaki siku ya tarehe 9 Agosti, ambalo liliwauwa watu 75,000 hapo hapo. Japan ilijisamilisha siku sita baadaye na hivyo kuhitimisha Vita vya Pili vya Dunia. 

Meya Tomihisa Taue wa Nagasaki alisema Japan inakaribia kufikia enzi mpya ikiwa na manusura wachache vikongwe wa mashambulizi hayo wanaoweza kuwasimulia kizazi cha sasa historia yao. Meya huyo alitaka ukweli huo kuchukuliwa kama indhari kwamba dunia inapaswa kuishi bila ya silaha za kinyuklia.

"Nadhani ni jambo la kimaumbile kwa Japan, taifa pekee lililowahi kupata uzoefu wa kupigwa bomu la nyuklia, kudhamiria kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia. Lakini ukweli ni kwamba Japan iko chini ya mwamvuli wa nyuklia wa Marekani. Njia moja mahsusi ya kuondokana na hali hii na kufikia dunia isiyo silaha za nyuklia ni dhana ya kuwa na eneo lisilo nyuklia," alisema meya huyo.

Waziri Mkuu Shinzo Abe alihudhuria kumbukumbu hiyo kama kawaida, lakini wageni kutoka jumuiya ya kimataifa walikuwa wachache. Mahudhurio ya mwaka huu yalikuwa asilimia 10 tu ya mahudhurio ya kawaida, ambapo viti vilitenganishwa kwa madaya ya kutosha huku watu wakiwa wamevaa barakowa.