Wanawake wa Korea walidhalilishwa kingono
2 Novemba 2015Maamzi hayo yanayoonekana kuwa ya kipekee kwa aina yake yanakuja baada ya mahusiano mabaya ya muda mrefu yaliyokuwepo kati ya mataifa hayo mawili.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema ya kwamba nchi yake inataka kuwepo kwa azimio la haraka iwezekanavyo kuhusiana na suala ikiwa ni muda mchache mara tu baada ya kukutana na Rais wa Korea Kusini Park Geun-hye.
Wanawake wa Kikorea walidhalilishwa kingono baada ya kulazimishwa kufanya mapenzi na wanajeshi wa Kijapan wakati Korea kusini ilipokuwa chini ya himaya ya Japan, tangu mwaka 1910 hadi Japan iliposhindwa katika vita kuu ya pili ya dunia mnamo mwaka 1945.
Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Korea kusini inasema , Rais wa nchi hiyo ambaye tangu aingie madarakani mnamo mwaka 2013, amekuwa akipigania juu ya fidia kutokana na udhalilishaji huo, amekubaliana na Waziri mkuu wa Japan juu ya kulimaliza suala hilo haraka iwezekanavyo.
Japan yasema suala hilo lilikwishapatiwa ufumbuzi
Japan imekuwa ikiendelea kusisitiza ya kuwa suala hilo tayari lilikwishamalizika tangu mwaka 1965 ambapo Japan ilipaswa kuilipa Korea kusini pesa zenye thamani ya sarafu ya euro 725 milioni ambazo ni sawa na dola za kimarekani milioni 800.
Hata hivyo Korea ya Kusini imeendelea kusisitiza ya kuwa Abe na viongozi wengine wa Japan waliopita walionekana kushindwa kulishughulikia barabara suala hilo.
Kikao cha jumatatu wiki hii kati ya viongozi hao kilikuwa ni kikao cha kwanza na cha aina yake kati ya viongozi hao tangu Abe aingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2012 na Park mapema mwaka 2013.
Abe amesema yeye pamoja na Park wamekubaliana pia juu ya mzozo unaofukuta katika bahari ya kusini ya China.
Katika siku za hivi karibuni Japan na China zimekuwa zikizozana juu ya visiwa visivyokaliwa na watu wakati China pia ikiendelea kudai baadhi ya maeneo katika ukanda huo yanayoshikiliwa na washirika wa Marekani kama vile Ufilipino.
Kikao cha jumatatu kati ya Bw. Abe na Park ambacho kilidumu kwa saa zisizopungua mbili kilitanguliwa pia na mkutano uliofanyika mjini Seoul hapo jumapili ambao pia ulimhusisha Waziri mkuu wa China, Li Keqiang , kikiwa ni kikao cha kwanza cha aina yake katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.
Mwandishi :Isaac Gamba/DW.
Mhariri :Yusuf Saumu