1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la njaa lainyemelea Yemen

Admin.WagnerD25 Juni 2015

Nchi ya Yemen ambayo ni maskini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu, iko hatarini kutumbukia kwenye janga la njaa baada ya mzozo wa miezi mitatu. Tahadhari hiyo imetolewa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen.

https://p.dw.com/p/1FnPK
Mjumbe maaluim wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed.
Mjumbe maaluim wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed.Picha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

" Tuko hatua moja,hatua moja kutoka hali ya kukabiliwa na njaa Tuna zaidi ya Wayemen milioni 21 wanaohitaji msaada wa kibinadamu hivi leo. Ukilinganisha kiwango hicho na wakati nilipokuwa mratibu wa misaada ya kiabinaadamu ilikuwa ni milioni saba na tena miaka miwili tu iliopita.Sasa tuna milioni 21." Hii ni kauli iliyotolewa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Sheikh Ahmed wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New York makao makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kukutana kwa faragha na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuliarifu juu ya hali ya Yemen.

Mjumbe huyo amezilaumu pande zote mbili katika mzozo wa Yemen kuhusika na mateso makubwa yanayowakabili wananchi wake hadi hapo nchi hiyo itakapoweza kuwa na usitishaji wa mapigano wa kweli.

Janga la kibinaadamu

Janga la kibinaadamu nchini Yemen limezidi kuongezeka wakati mzozo nchini humo ukipamba moto.Mapigano ya ardhini na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kishia wa jamii ya Wahouthi Jumatano yameuwa takriban watu 100.

Mtoto wa Yemen.
Mtoto wa Yemen.Picha: DW/A. Stahl

Mzozo huo umesababisha watu milioni 20 kukosa maji safi ya kunywa na kuwapotezea makaazi wengine zaidi ya milioni moja.

Kuzifungia badari za Yemen imefanya iwe vigumu sana kufikisha misaada ya kibinaadamu nchini humo.Lakini Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu imesema meli yenye kubeba tani 1,000 za chakula na magenereta matatu makubwa imefunga gati katika bandari ya Hodeida hapo Jumatano.

Wakati kuwasili kwa meli hiyo ni habari za kutia moyo nadra kusikika nchini humo, mapigano yameanza mapema alfajfiri hapo Jumatano katika miji ya Ibb, Aden, Taiz, Marib, Dhale na ngome kuu ya Wahouthi huko Saada na kuuwa takriban watu 100 wakiwemo raia wengi.

Juhudi za usuluhishi

Mjini Aden makombora kadhaa yameangukia kwenye vitongoji vyenye wakaazi wengi wakati mashambulizi ya mizinga yamekuwa yakiutingisha mji wa Taiz.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati wa mazungumzo ya amani ya Yemen mjini Geneva.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati wa mazungumzo ya amani ya Yemen mjini Geneva.Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Gillieron

Katika juhudi za kutafuta suluhu maafisa wa usalama wa Yemen wamesema wawakilishi wa vuguvugu linalotaka kujitenga la kusini mwa nchi hiyo wanakutana na Wahouthi katika mji mkuu wa Oman,Muscat.

Ujumbe kutoka chama cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh pia inatajwa kwamba umeelekea Moscow kukutana na maafisa wa serikali ya Urusi.Zaidi ya watu 2,600 wameuwawa nchini Yemen tokea mwezi wa Machi na takriban asilimia 80 ya idadi ya watu wa nchi hiyo milioni 20 wanahitaji msaada wa kibinaadamu wa dharura.

Mazungumzo ya amani yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kati ya waasi na maafisa wa serikali yalimalizika Geneva wiki iliopita bila ya kufikiwa kwa makubaliano.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters

Mhariri : Iddi Ssessanga