1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la Corona latishia kurudisha nyuma masuala ya afya

Saleh Mwanamilongo
25 Septemba 2020

Ripoti ya Umoja wa mataifa imesema janga la virusi vya corona linatishia kurudisha nyuma hatua za muongo zilizopigwa katika masuala ya afya ya wanawake na watoto.

https://p.dw.com/p/3j0vs
Pressefoto UNHCR | Syrien, Idlib
Picha: UNHCR/Gordon Welters

Ripoti hiyo imeangazia hatua kubwa zilizopigwa tangu kulipoanzishwa mkakati ya Umoja wa Mataifa wa Kila Mwanamke, Kila Mtoto miaka kumi iliyopita, unaohusisha pamoja na mambo mengine, chanjo kwa watoto zaidi ya bilioni moja na kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano katika kiwango cha chini kabisa ifikapo mwaka 2019.

Ripoti hiyo aidha imeonya iwapo hakutachukuliwa hatua za makusudi za kukabiliana na vifo vinavyozuilika, watoto milioni 48 wa chini ya miaka mitano huenda wakafariki dunia kati ya mwaka 2020 na 2030.

Takwimu za shirika la habari la AFP Ijumaa, zinaonyesha kuwa janga la virusi vya Corona limeuwa watu zaidi ya laki tisa na themanini na nne elfu (984.048) kote ulimwenguni.

Maambukizi yakiwa zaidi ya watu milioni 32 toka kuanza kwa janga hilo,huku watu waliopona wakifikia zaidi ya milioni 22.

Nchi zilizoorodhesha idadi kubwa ya vifo mnamo masaa 24 iliyopita ni pamoja na India  vifo 1,141, Marekani  na vifo 846 na Brazil ikiwa na vifo 831.