1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika ya Kati yasema imewauwa waasi 44

26 Januari 2021

Jamhuri ya Afrika ya Kati imesema majeshi yake yamewaua waasi 44 wanaopambana kutaka kuuzingira mji mkuu Bangui, kwa lengo la kuupindua utawala wa rais aliyechaguliwa tena hivi karibuni Faustin Archange Touadera.

https://p.dw.com/p/3oPyV
Zentralafrikanische Republik
Picha: Nacer Talel/AA/picture alliance

Siku ya Jumatatu serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iliandika katika mtandao wake wa Facebook kwamba vikosi vyake kwa kushirikiana na vikosi vya washirika wao wameanzisha operesheni kwenye kijiji cha Boyali kilichopo umbali wa kilomita 90 kutoka kwenye mji mkuu, huku upande wa serikali ukiwa haujapata madhara na imeongeza kusema kuwa waasi 44 wameuawa wakiwemo mamluki kutoka Chad, Sudan na wapiganaji wa kabila la Fulani.

Nchi hiyo inapozungumzia majeshi washirika inamaanisha wale kutoka Rwanda na Urusi ambao walipelekwa nchini humo. Msemaji wa serikali, Ange-Maxime Kazagui ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba vikosi vya serikali vimerejea kwenye mapambano na kwa msaada wa wapiganaji wa Urusi, wamefanikiwa kukidhibiti kijiji cha Boda kilichopo umbali wa kilomita 124 kutoka Bangui.

Soma zaidi: Waasi wauteka mji wa Bangassou Jamhuri ya Afrika ya Kati

Makundi sita yenye silaha na yenye nguvu zaidi nchini humo ambayo yalikuwa yanadhibiti theluthi mbili ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mzozo wa miaka minane, yalijiunga mwezi Desemba na kuanzisha muungano unaojulikana kama Ushiriki wa Wazalendo kwa ajili ya Mabadiliko, CPC. Desemba 19 muungano huo mpya ulitangaza kuanzisha mashambulizi mjini Bangui kwa lengo la kumzuia Touadera kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa urais uliofanyika Desemba 27.

Hata hivyo, mji huo mkuu ulikuwa unalindwa na wanajeshi 12,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, MINUSCA wenye vifaa imara, pamoja na majeshi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na vikosi kutoka Urusi na Rwanda.

Siku ya Jumatatu serikali ilitangaza kuhusu kufanikiwa katika shambulizi, ambalo shirika la habari la AFP halikuweza kuthibitisha na vyanzo huru, na ni mara ya kwanza viongozi wametoa taarifa sahihi kuhusu majeruhi wa vikosi vingine isipokuwa wanajeshi wa MINUSCA. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa waasi wanajaribu kuuzingira mji mkuu kwa kuzuia barabara kuu zinazoelekea huko.

Niederlande Den Haag Internationaler Strafgerichtshof | Fatou Bensouda
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC, Fatou BensoudaPicha: Getty Images/AFP/ANP/E. Plevier

Wakati huo huo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC Fatou Bensouda amepongeza hatua ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita, Mahamat Said Abdel Kani, ingawa amesema bado ana wasiwasi kuhusu hali mbaya ya nchi hiyo.

''Ninapongeza hatua ya kuhamishiwa mtuhumiwa Bwana Mahamat Said Abdel Kani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kukabiliana na mkono wa sheria kutokana na madai ya uhalifu kama alivyoshtakiwa kabla na ICC. Ninawashukuru wote waliofanikisha suala hili,'' alifafanua Bensouda.

Kani anayedaiwa kuwa kiongozi wa muungano wa waasi wa Seleka, uliokuwa na Waislamu wengi alikabidhiwa kwa mahakama ya ICC siku ya Jumapili na aliwasili katika kitengo cha mahabusu cha mahakama hiyo mjini The Hague Jumatatu asubuhi.

Kani, mwenye umri wa miaka 50 anatuhumiwa kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita, ikiwemo utesaji baada ya nchi hiyo kutumbukia katika ghasia za kidini mwaka 2013, kutokana na kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozize.

(AFP)