Jamhuri ya Afrika ya Kati: Bozize arejea nyumbani
17 Desemba 2019Chama cha rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize kimesema kiongozi huyo amerudi nyumbani baada ya takriban miaka saba ya kuishi uhamishoni.
Bozize aliondolewa madarakani na kundi la muungano wa waasi mnamo mwezi Marchi mwaka 2013, na amekuwa akiishi nchini Uganda.
Katibu mkuu wa chama chake Bertzin Bea amewaambia waandishi habari jana Jumatatu kwamba Bozize anapanga kulihutubia taifa katika siku kadhaa zijazo.
Hata hivyo Bea hakueleza kuhusu Bozize alivyorudi nchini lakini mahakama ya nchi hiyo, hivi karibuni iliondowa amri ya kuyazuia mashirika ya ndege kumsafirisha Bozize kwenda Bangui.
Wafuasi wa Bozize wanasema kuondolewa kwake kwa nguvu madarakani kulifungua kipindi mojawapo kibaya cha vurugu katika historia ya nchi hiyo.
Wengine wana hofu kuwa kurejea kwake kunaweza kusababisha mvutano zaidi wa kisiasa kabla ya uchaguzi wa mwakani.