1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika Kati Wiki hii Magazetini

14 Machi 2014

Jamhuri ya Afrika kati ,kesi ya Oscar Pistorius na ukosefu wa umeme nchini Afrika kusini na ndovu wa Afrika wenye kutofautisha watu kutokana na sauti zao ni miongoni mwa mada katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

https://p.dw.com/p/1BPll
Padri Benedyk Paczka akizungukwa na watoto huko Ngaoundaye,katika jamhuri ya Afrika katiPicha: Benedykt Paczka

Tunaanzia jamhuri ya Afrika kati ambako hali inayotisha iliyoenea nchini humo imeendelea kugonga vichwa vya habari wiki hii."Hofu na wasi wasi umeenea" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la Die Zeit linalosema dini sio chanzo cha mgogoro.Ripota wa gazeti hilo anasema kwa miezi sasa ripoti zinazungumzia vita kati ya waislam na wakristo-pengine anasema ripota huyo, nchi za magharibi zinahitaji picha kama hiyo kuweza kuelewa kinachotokea,lakini katika kadhia ya Jamhuri ya Afrika kati picha hiyo si ya kweli.Mauwaji yanayoendelea tangu decemba mwaka jana hayahusiani hata kidogo na dini.Lakini chuki hii inatokea wapi anajiuliza ripota wa gazeti hilo la Die Zeit ambae binafsi amekulia katika jamhuri ya Afrika kati kama mtoto wa wamishionari.Anaelezea wakati walipokuwa watoto,wakicheza pamoja na wenzao vichakani na majumbani,na kula mihogo na vyakula vyengine vya kienyeji.Anaelezea jinsi walivyokuwa shuleni .Jinsi watu walivyokuwa wakiishi pamoja kwa wema.Hakuna anaeuwa kwasababu ya dini yake anasema na kujiuliza matumizi haya ya nguvu yanasababishwa na nini?Kuna sababu mbili anasema ya kwanza matumizi ya nguvu yanaangaliwa kama njia ya kurejesha suluhu kwa maneno mengine damu ikimwagika na shetani atatoweka.Sababu ya pili anasema ni hofu.Anasema katika jamhuri ya Afrika kati,hofu inawafanya watu wadanganyike.Kinachohitajika kwasasa anasema ripota wa die Zeit ni kurejesha sheria na nidhamu na badala ya kulenga zaidi dini,nchi za magharibi zinapaswa kusaidia kuijenga upya nchi hiyo,ikiwa ni pamoja na kuipatia misaada ya fedha serikali ya jamhuri ya Afrika kati ili iweze kuwajibika ipasavyo.Walimwengu wanabidi watambue utulivu hautarejea kufumba na kufumbua panahitahjika mkakati wa ujenzi madhubuti wa nchi hiyo.Anamaliza kuandika Silvia Kuntz wa gazeti la Die Zeit.

Ukosefu wa Umeme Afrika Kusini

Kesi ya mwanariadha mwenye ulemavu wa Afrika kusini Oscar Pistorius nayo pia imegonga vichwa vya habari.Gazeti la Frankfurter Allgemeine limezungumzia zaidi shida za umeme zilizovuruga matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kuhusu kesi hiyo.Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2008 kampuni la umeme la ESKOM limetangaza hali ya dharura baada ya kushindwa kukidhi mahitaji jumla ya umeme nchini humo.ESKOM limeweza kukidhi asili mia 90 tu ya mahitaji ya umeme,majimbo tangu wiki iliyopita yanapatiwa umeme kwa zamu.Makampuni yanayotumia umeme kwa wingi yamearifiwa tangu mapema mwaka huu yanabidi yapunguze kwa asili mia 10 matumizi yao ya nishati.Ingawa kuanzia wiki hii hali imeanza kutulia hata hivyo kupitia mitandao ya kijamii watu wanaonya kuhusu hatari kubwa ya kujikuta bila ya umeme.Frankfurter Allgemeine linanukuu maoni ya wanauchumi wanaohisi matatizo ya umeme yanahatarisha ukuaji wa kiuchumi ambao tokea hapo ni dhaifu.Kuanzia Johannesburg hadi kufikia Cape Town watu wanawasha mishumaa kwasababu kila siku usiku wanakaa kizani.Eskom linahoji hali ya hewa n dio chanzo cha matatizo ya kuzalisha umeme.Mvuwa kali ya wiki nzima imerovya akiba ya makaa mawe ya kinu cha umeme.Zaidi ya hayo kuna vifaa vya kinu kimoja cha umeme vilivyoharibika.Na kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Afrika Kusini kuna uhaba wa karibu thuluthi moja ya ugavi wa nguvu za umeme kwasasa nchini humo.Bei ya umeme imepanda mara tatu ikilinganishwa na mwaka 2008 na hiyo ndio sababu mahitaji yamepungua.

Wewe Nani ,muulitze Ndovu

Na hatimae lilikuwa gazeti la Süddeutsche lililoandika kuhusu ndovu wa Afrika wanaotofautisha watu kutokana na sauti zao.Anaeita ni mwanamme au mwanamke?Ni mmasai au mkamba?Süddeutsche Zeitung limemnukuu mtaalam wa kisayansi aliyeliandikia jarida la PNAS akisema ndovu wa Afrika wanaweza kutofautisha yote hayo wanapoisikia sauti tu ya mtu.Wanyama hao wanaweza kutofautisha umri,jinsia na hata kabila la mtu kutokana na sauti yake.Tangu zamani ilikuwa ikitajwa kwamba ndovu wanatambua kabila la mtu kutokana na umbo na harufu.Uchunguzi huu mpya umefanyika katika mbuga ya wanyama ya Amboseli nchini Kenya.Kundi la wataalam waliongozwa na Karen McCombo wa chuo kikuu cha Sussex limeelezea jinsi ndovu walivyokuwa wakijikusanya kwa woga na hata kurejea nyuma wanaposikia sauti ya mwanamme na jinsi walivyokuwa wakionyesha wamepowa waliposikia sauti ya wanawake na watoto.Kauli iliyotumiwa kufanya uchunguzi huo,linaandika Süddeutsche Zeitung "Angalia,angalia nyuma,ndovu wanakuja."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman