Jakarta yatikiswa na mashambulizi ya kigaidi
14 Januari 2016Wakati kidole cha lawama kinaelekezwa kwa kundi hilo la Dola la Kiislamu au washirika wake, polisi imesema hawajui nani amehusika na mashambulizi hayo, na rais Joko Widodo ameutaka umma kutoanza kukisia juu ya nani anahusika.
Polisi imesema kulikuwepo na mashambulizi yasiyopungua sita, na kwamba waliwapiga risasi na kuwauwa washambuliaji watatu na kuawakamata wengine wanne. Waripuaji watatu wa kujitoa muhanga wanashukiwa kushiriki, na maafisa polisi watatu na raia watatu wameuawa pia.
Mashambulizi hayo yamelilenga jengo la ofisi na yalianza na mripuko nje ya mkahawa wa Starbuck uliyoko kwenye gorofa ya chini ya jengo hilo, ambao vioo vya madirisha yake vimepasuka kutokana na kishindo.
'Hatutatishiwa na magaidi'
Mashambulizi hayo ya Alhamis hayakuja kama mshangao kwa viongozi wa Indonesia, ambao walionya mwezi Desemba juu ya kitisho cha kweli. Serikali ilikuwa imeweka askari 150, 000 kulinda makanisa, viwanja vya ndege na maeneo mengine ya umma katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi, na kuendesha msako wa kuzuwia dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
Rais Joko Widodo alikuwa nje ya mji wa Jakarta wakati mashambulizi hayo yakifanyika, lakini amekatiza ziara yake na kurudi katika mji huo wa wakaazi milioni 10 kusimamia mwenyewe operesheni hiyo.
"Hatupaswi kuogopa, tusikubali kushindwa na kitendo cha magaidi kama hiki, na ni matumaini yangu kwamba watu wanasalia kuwa watulivu kwa sababu hali hii inadhibitika," alisema rais Widodo katika mazungumzo na waandishi wa habari.
Indonesia ilikumbwa na mashambulizi kadhaa makubwa yanayofanywa na Waislamu wenye itikadi kali kati ya mwaka 2000 na 2009, yakiwemo mashambulizi ya mwaka 2002 kwenye kisiwa cha mapumziko cha Bali, ambayo yaliuwa watu 202. Operesheni ya vikosi vya usalama iliyoendeshwa baadae iliidhoofisha mitandao hatari, na kuepelekea kusimama kwa muda mrefu, mashambulizi ya kiwango kikubwa.
Hofu ya wapiganaji wa IS wanaorejea
Lakini la Soufan lenye makao yake Ulaya, linasema baadhi miongoni mwa wa Indonesia 500 hadi 700 waliokwenda nje kujiunga na kundi lililojitangazia ukhalifa la Dola la Kiislamu wamerejea nchini humo.
"Tunafahamu kwamba IS wana shauku ya kutangaza mkoa katika kanda hii," alisema Kumar Ramakrishna, mchambuzi wa mapambano dhidi ya ugaidi kutoka shule ya masuala ya kimataifa ya S. Rajaratnam nchini Singapore.
Pamoja na vifo vilivyothibtishwa, watu kadhaa wengine wanahofiwa kujeruhiwa, ambapo shuhuda wa shirika la habari la Ufaransa AFP, alisema alimuona gaidi akiwamiminia risasi za mfululizo wapita njia, akiwemo mwandishi wa habari wa ndani.
Eneo yalikotokea mashambulizi hayo ndiyo makao ya balozi kadhaa za kigeni, zikiwemo za Marekani, Ufaransa na Uhispania. Mashrika kadhaa ya Umoja wa Mataifa pia yanakutikana katika maeneo ya jirani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre,ape
Mhariri: Saumu Yusuf