1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji aamuru Rais al -Bashir asiondoke Afrika Kusini

14 Juni 2015

Hakimu wa Afrika Kusini ameamuru serikali ya nchi hiyo kumzuwiya Rais Omar al- Bashir wa Sudan ambaye yuko Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika kuondoka nchini humo..

https://p.dw.com/p/1Fh5b
Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan mjini Johannesburg. (14.06.2015)
Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan mjini Johannesburg. (14.06.2015)Picha: Reuters/S. Sibeko

Jaji Hans Fabricuis amerefusha amri ya kuzuwiya kuondoka kwa rais huyo hadi hapo itakapotowa maamuzi ya mwisho Jumatatu na kuitaka serikali kuchukuwa hatua zote muafaka kumzuwiya la Bashir al- Bashir asiondoke nchini humo.

Fabricius ameagiza vituo vyote vya udhibiti wa mipaka nchini Afrika Kusini vijulishwe juu ya amri hiyo ili kuhakikisha kwamba al- Bashir hawezi kuondoka kabla ya kutolewa hukumu.

Al- Bashir ameonekana akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Kiafrika katika mkutano huo wa kilele mjini Johannesburg Jumapili (14.06.2015) akivalia suti ya rangi ya buluu na kutabasamu wakati wakipigwa picha.

Bashir awekewa kinga

Chama cha ANC ambacho ndio chama tawala nchini humo kimesema serikali ya Afrika Kusini imewaekea kinga ya kutokamatwa washiriki wote wa mkutano huo wa kilele ikiwa kama ni kanuni ya kimataifa kwa nchi zenye kuandaa mikutano hiyo ya Umoja wa Afrika au hata Umoja wa Mataifa.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini (kulia) akiwa na viongozi wa nchi za Kiafrika,
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini (kulia) akiwa na viongozi wa nchi za Kiafrika,Picha: picture-alliance/dpa/Gcis/Siyasanga Mbambani

Chama hicho kimesema kwamba kwa msingi huo miongoni mwa mambo mengine ANC inaitaka serikali kupinga amri hiyo inayoilazimisha serikali ya Afrika Kusini kumkamata Rais al Bashir na kuongeza kusema kwamba nchi za Kiafrika na Ulaya ya Mashariki zinaendelea kubebeshwa maamuzi ya mahakama hiyo ya ICC pasipo haki.

Hata kabla ya mkutano huo wa Jumapili Umoja wa Afrika ulikuwa umeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kusitisha mchakato wa kesi zake dhidi ya marais wanaokuwa madarakani na kusema kwamba haitolazimisha nchi yoyote mwanachama kumkamata kiongozi kwa niaba ya mahakama hiyo.

Al- Bashir amekuwa akisafiri nchi za nje hapo kabla na hakuna serikali ya kitaifa iliomkamata kwa niaba ya mahakama ya ICC yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi.

Wajibu wa kisheria

Kituo cha Haki za Kisheria cha Kusini mwa Afrika ambalo ni shirika la haki za binaadamu limesema limepata hukumu ya jaji yenye kuilazimisha serikali kumzuwiya al Bashir kuondoka Afrika Kusini wakati mahakama ikisikiliza hoja za kutaka akamatwe kwa madai ya mauaji ya kimbari na vitendo vyengine vya kihalifu.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC Fatou Bensouda .
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC Fatou Bensouda .Picha: AFP/Getty Images

Mwendesha mashtaka wa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu Fatou Bensouda amesema Afrika Kusini ina wajibu wa kisheria kumkamata na kumsalimisha al Bashir kwa mahakama hiyo ya ICC.Ofisi yake imekuwa katika mawasiliano na serikali ya Afrika Kusini kuhusiana na ziara hiyo ya rais wa Sudan.

Iwapo al- Bashir hatokamatwa suala hilo litafikishwa kwa baraza la nchi wanachama wa mahakama hiyo na kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo ndio lililofikisha kesi ya jimbo la Dafur nchini Sudan kwa mahakama ya ICC hapo mwaka 2005.

Mzozo wa Dafur

Mashtaka dhidi ya al- Bashir ambaye ameingia madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1989 yanatokana na unyama ulioripotiwa katika mzozo wa Dafur ambapo watu 200,000 wameuwawa na wengine milioni mbili wamepotezewa makaazi yao kutokana na mashambulizi ya serikali.

Wakimbizi wa Dafür nchini Sudan.
Wakimbizi wa Dafür nchini Sudan.Picha: AP

Rais huyo wa Sudan tayari ametembelea Malawi,Kenya, Chad na Congo miaka michache iliopita nchi ambazo zote ni wanachama wa mahakama ya ICC.Mahakama hiyo haina nguvu yoyote ile ya kuzilazimisha nchi kumkamata kiongozi huyo na inaweza tu kuzieleza kwamba zina wajibu wa kisheria kufanya hivyo.

Sudan imesisitiza kwamba ziara ya rais wao nchini Afrika Kusini inaendelea vyema na atarudi nyumbani baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika.

Mwandishi : Mohamed Dahman Reuters/AP/AFP

Mhariri : Bruce Amani