Italia yajikwaa, Ufaransa yafanya kweli
22 Juni 2014Kwa kipigo hicho Italia mabingwa mara nne wa kombe la dunia imejiweka katika ukingo wa kuyaaga mashindano haya na mapema. Lakini Ufaransa haikufanya mzaha kabisa na imeikandika Uswisi mabao 5-2 katika pambano ambalo Ufaransa imeonesha uwezo mkubwa.
Baada ya mshangao mwingine katika kombe hili la dunia nchini Brazil, ushindi wa Costa Rica umeiweka timu hiyo katika nafasi ya kwanza katika kundi D na hatua hiyo inamaana kwamba Uingereza, imeyaaga mashindano haya baada ya michezo miwili, wakati Italia na Uruguay sasa zitalazimika kupambana kufa kupona katika mchezo wao wa mwisho siku ya Jumanne wiki ijayo.
Luis Suarez atakuwa fit kwa mchezo huo, ikiwa ni nafasi nzuri kwa Uruguay baada ya mshambuliaji huyo kupachika mabao yote mawili dhidi ya Uingereza juzi.
Bao lililoizamisha Italia
Mpira uliozamishwa kwa kichwa wavuni na Bryan Ruiz katika kipindi cha kwanza ulitenganisha timu hizo mbili, na kuwaacha mashabiki wa Costa Rica walishangiria na kucheza katika uwanja wa mjini Recife wa Pernambuco baada ya kupata ushindi wa pili katika michezo miwili.
Kocha wa Italia Cesare Prandelli ameeleza matumaini kabla ya pambano dhidi ya Uruguay ,ambapo kikosi chake kinahitaji sare tu kuweza kuvuka awamu hii na kuingia awamu ya mtoano ya timu 16 kutokana na kuwa na tofauti nzuri ya magoli.
Ufaransa iliishinda Uswisi kwa mabao 5-2, katika mchezo wa kupendeza, wa vuta nikuvute ulikuwa na nafasi kadha za mabao na ambao ulikuwa wa kupendeza mno kwa shabiki ambaye haelemei upande wowote.
Maumivu kwa kocha Hitzfeld
Kwa kocha wa Uswisi Ottmar Hitzfeld ni hali ya kuumiza wakati akiangalia ukuta wa kikosi chake ukivunjwa na wimbi baada ya wimbi la mashambulizi kutoka kwa washambuliaji wa Ufaransa.
Ushindi huo wa kishindo umeendeleza ukarabati unaoendelea wa kikosi cha Ufaransa wakati wakiwania kuzika mzuka wa miaka minne iliyopita, wakati wachezaji walipoasi na kuchafua hadhi yao.
"Ulikuwa mchezo mzuri sana , tulifanya mambo mengi kwa usahihi," amesema kocha wa Ufaransa Didier Deschamps katika mahojiano.
Matokeo hayo yameiweka Ufaransa juu ya msimamo wa kundi E ikiwa na points 6, mbele ya Ecuador ambayo ina points tatu. Kundi hilo bado liko wazi , hata hivyo, ambapo Ecuador iliishinda Honduras kwa mabao 2-1 mjini Curitiba. Timu mbili zina points sawa , Uswisi na Ecuador, lakini Ecuador ikiwa na tofauti nzuri ya mabao.
Argentina na Messi
Leo jioni(21.06.2014) Leonel Messi na kikosi cha Argentina watawania kukata tikiti yao katika timu 16 bora za kombe la dunia mwaka huu nchini Brazil katika mchezo dhidi ya Iran katika uwanja wa Mineiro. Baada ya hapo itakuwa zamu ya Ghana kujaribu bahati ya timu za Afrika kuweza kuingia katika duru ya mtoano ya timu 16.
Ghana inapambana na Ujerumani inayopigiwa upatu kutoroka na kombe hili. Ujerumani inaweza kukata tikiti yake kuingia katika timu 16 bora iwapo itaishinda Ghana katika mchezo wa kundi G.
Mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Nigeria na Bosnia. Nigeria ikiwa na point 1 baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Iran , inakutana na Bosnia, ambayo haina point baada ya kuangushwa na Argentina kwa mabao 2-1, wakitafuta ushindi ili kuendeleza matumaini ya kushika nafasi ya pili katika kundi F.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae