Italia yaingia katika mdororo wa kiuchumi
31 Januari 2019Wakati huo huo kasi ya ustawi wa uchumi wa mataifa ya kanda ya sarafu ya euro imepungua sana hadi asilimia 1.8 katika mwaka 2018.
Data zinaonesha kwamba kupungua kwa mauzo ya nje nchini Ujerumani na wasi wasi kuhusiana na kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit kumepunguza kasi hiyo kwa kiasi kikubwa. Uchumi wa Italia , ukiwa ni uchumi wa tatu mkubwa katika kanda ya sarafu ya euro , ulinywea kwa kiwango cha kipindi cha robo mwaka kwa asilimia 0.2 katika robo ya nne ya mwaka 2018, limesema shirika la takwimu la taifa nchini Italia.
Kufuatia kuporomoka kwa asilimia 0.1 katika vipindi vya miezi mitatu ya nyuma hii ina maana Italia imo kimsingi katika hali ya mdororo wa kiuchumi, inayotafsirika kuwa ni vipindi viwili mfululizo vya kunywea kwa uchumi kiasi ya miaka minne baada ya hali hiyo kutokea mara ya mwisho.
Mdororo wa kiuchumi nchini Italia ni sababu mojawapo kwanini kanda hiyo ya euro ilipungua kasi katika ukuaji wake wa uchumi katika mwaka 2018, pamoja na hali ya sintofahamu inayohusiana na Brexit, mzozo wa kiuchumi kati ya China na Marekani pamoja na viwango vipya vya utoaji wa gesi chafu kwa magari.
Shirika la takwimu
Licha ya kuwa kanda ya euro inafanya vizuri kuliko katika nyakati za giza za mzozo wa madeni , ambao ulitishia kuvunjilia mbali umoja huo wa sarafu, bado uchumi wake uko nyuma ya Marekani, ambayo ilitabiriwa kukua kwa asilimia 3 katika mwaka 2018. Kutokana na hayo , ukosefu wa ajira katika kanda ya sarafu ya euro ni kiasi ya mara mbili ya asilimia 4 ya Marekani inayofikia asilimia 7.9.
Uchumi wa kanda ya sarafu ya euro ulikuwa kwa jumla ya asilimia 0.2 tu katika robo ya mwisho ya mwaka 2018, sawa kama katika robo iliyopita ya mwaka, kwa mujibu wa tarakimu za awali zilizotolewa leo na shirika la takwimu la Eurostat.
Uchumi huo umepanuka kwa asilimia 1.8 katika mwaka 2018 kwa jumla , ikiwa ni kiwango chake dhaifu kabisa katika muda wa miaka minne. Hii ni chini kuliko ilivyotarajiwa mwaka mmoja uliopita, wakati kundi hilo la mataifa lilipotarajiwa kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kiasi kidogo kutoka ukuaji mkubwa wa mwaka 2017 wa asilimia 2.4.
Uchumi wa Italia umekuwa chachu ya chanzo cha wasi wasi katika muda wa miezi michache iliyopita, kwa sehemu fulani ikiwa ni matokeo ya msuguano wa serikali mpya ya siasa za kizalendo na halmashauri ya Umoja wa ulaya kuhusiana na mipango ya bajeti yake, hali ambayo imedhoofisha imani ya wafanyabiashara na kushuhudia viwango vya kukopa katika masoko ya hisa vya Italia vikiongezeka kwa kiwango cha juu kabisa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Idd Ismail Ssessanga