1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia, Ujerumani zafunguwa tena mipaka

3 Juni 2020

Maisha yanaendelea kurudi kuwa ya kawaida Ulaya kwa baadhi ya mataifa kufunguwa mipaka na kuondosha marufuku ya kusafiri, lakini athari za kiuchumi za zuwio lililokuwepo huenda zikawa za muda mrefu zaidi ujao.

https://p.dw.com/p/3dBQ3
Deutschland | Flughafen Hamburg | Lufthansa | Germanwings
Picha: imago images

Ujerumani imetangaza kwamba itaondowa ushauri wa kuzuwia safari kwa mataifa ya Ulaya ifikapo tarehe 15 mwezi huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje, Heiko Maas, uamuzi huo unayahusu mataifa yote wanachama wa Umoja wa Ulaya, pamoja na nchi chache kwenye eneo hili, zikiwemo Uswisi na Iceland. 

Lakini Italia imeamuwa kuchukuwa hatua hiyo leo kwa kuifunguwa tena mipaka yake kwa ajili ya wageni kutoka mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya na kuondoa marufuku ya kusafiri kati ya mikoa yake yenyewe.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Italia, Luigi Di Maio, ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba Jumatano ya leo ni siku muhimu kwani nchi inaanza upya maisha yake na imepania kurejea kwenye hali ya kawaida.

Italia ilizuia rasmi shughuli zote za kawaida za maisha tarehe 10 Machi, na tangu mwezi uliopita hatua za kuondowa zuio zimekuwa zikichukuliwa kidogo kidogo, ingawa bado agizo la kuweka masafa baina ya watu linaendelea kutekelezwa. 

Shinikizo la kuufunguwa tena uchumi

Italien Corona-Pandemie Flashmob Schiefer Turm Von Pisa
Muziki wa umma kwenye uwanja wa Miujiza, Pisa, nchini Italia kuadhimisha kufunguliwa tena kwa shughuli za umma.Picha: picture-alliance/NurPhoto/E. Mattia Del Punta

Kulegezwa huku kwa hatua za kudhibiti maambukizo ya virusi vya korona, kunakuja kutokana na kushuka sana kwa idadi ya maambukizo mapya na shinikizo kutoka kwa kampuni na wafanyakazi kutaka kufunguliwa upya kwa shughuli za kiuchumi na uzalishaji.

Hapa Ujerumani, kampuni zimelazimika kusaka uungwaji mkono wa serikali kwa ajili ya masaa machache kazini kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya milioni 11 tangu mwezi Machi.

Idadi ya wasio ajira ilipanda hadi asilimia 6.3 kwa mwezi uliopita wa Mei, ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwezi Aprili.

Kabla ya kuibuka kwa mripuko wa virusi vya korona, idadi ya wasio ajira japa Ujerumani haikuwahi kuvuuka asilimia 5 tangu mwezi Agosti 2018.

Sweden yajuta

Kwa upande mwengine, Sweden, taifa la Ulaya ambalo liliamua kuchukuwa njia tafauti ya kukabiliana na maambukizo ya virusi vya korona kwa kutokufunga shughuli zake za kawaida, imesema sasa kwamba uamuzi wake huenda uliwaweka wengi kwenye hatari zaidi.

Anders Tegnell, mkuu wa shirika la afya la nchi hiyo, amekiambia kituo kimoja cha habari hivi leo kwamba Sweden ilipaswa kufanya megi zaidi kuzuwia vifo ambavyo vimetokea.

Sweden limepoteza hadi sasa watu 4,500, idadi kubwa zaidi kuliko mataifa ya Denmark, Norway na Finland na imekuwa ikikosolewa sana kwa kutokufuata mfumo wa wenzao wa Ulaya kwenye udhibiti wa mripuko wa COVID-19.

Taifa hilo lilitegemea zaidi tabia ya watu wake kujiwekea masafa na kujisafisha kila mara.